1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawasiliano na wapiganaji wa Ukraine Azovstal yarejea

5 Mei 2022

Mbunge mmoja mwenye ushawishi katika bunge la Ukraine David Arakhamia amesema vikosi vya Urusi vimeingia katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichoko mjini Mariupol baada ya kufanya mashambulizi makali hapo Jumatano.

https://p.dw.com/p/4Aq3h
Rauch über dem Stahlwerk von Azovstal in Mariupol
Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Mbunge mmoja mwenye ushawishi katika bunge la Ukraine David Arakhamia amesema vikosi vya Urusi vimeingia katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kilichoko mjini Mariupol baada ya kufanya mashambulizi makali hapo Jumatano.

Arakhamia vile vile amesema kwa sasa mawasiliano na wanajeshi wa Ukraine walioko katika kiwanda hicho yamesharejea baada ya meya wa Mariupol Vadym Boichenko mapema Jumatano kusema kuwa wamepoteza mawasiliano na wanajeshi hao.

Kamanda mmoja wa Ukraine Denis Prokopenko amesema wapiganaji wa Ukraine katika kiwanda hicho wanakabiliana vikali na majeshi ya Urusi huku akidai mapigano hayo ni "magumu na yaliyo na umwagikaji wa damu."

Sheria za kimataifa za vita zakiukwa Ukraine

Mamlaka ya mji wa Mariupol imesema karibu raia 200 na zaidi ya watoto 30 bado wamekwama katika kiwanda hicho. Rais Volodymyr Zelenskiy naye amesema kunahitajika muda mrefu wa kusitisha mapigano mjini Mariupol ili shughuli ya uokoaji wa raia walioko mjini humo iweze kutekelezwa kikamilifu.

Ukraine-Krieg | Lage in Mariupol
Vifaru vya majeshi ya Urusi mjini MariupolPicha: Chingis Kondarov/REUTERS

Naye mkuu wa mpango wa uangalizi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine Matilda Bogner anasema sheria za kimataifa za vita hazizingatiwi katika vita hivyo. Bogner ameiambia DW kuwa idadi ya mashambulizi yaliyolenga maeneo walioko raia zikiwemo shule na hospitali inaonyesha wazi kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya silaha.

Bogner anasema Umoja wa Mataifa umerekodi zaidi ya vifo elfu tatu kwa sasa ila akaonya kwamba kuna uwezekano kwamba idadi kamili itakuwa juu zaidi kwani shughuli ya kupata ushahidi haikuwa rahisi kutokana na vifaa vyao vya uangalizi kutoweza kufika katika maeneo yanayodhibitiwa na majeshi ya Urusi.

Hayo yakiarifiwa Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema ataendelea kufanyamazungumzo na Rais Putin wa Urusi na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ila akadai kusiwe na matumaini makubwa ya kupatikana kwa amani kwa kuwa amani itapatikana tu iwapo Urusi itafikia makubaliano na Ukraine.

Urusi kuandaa gwaride Mariupol kuadhimisha "Siku ya Ushindi"

Ukraine inasema Urusi kwa sasa ina mpango wa kuandaa gwaride la ushindi wa Vita vya Pili vya Dunia mjini Mariupol mnamo Mei 9. Taarifa za kiintelijensia za jeshi la Ukraine zinasema majeshi ya Urusi inaisafisha mitaa ya kati ya mji huo kwa kuondoa vifusi, miili na mabomu ambayo hayajalipuka. Taarifa hizo pia zinasema Urusi inaandaa kampeni ya propaganda pia ambapo televisheni za Urusi zitaonyesha video za wakaazi wa Mariupol wakiwa na furaha kuwakaribisha wanajeshi wa Urusi mjini humo.

Ukraine | Eindrücke aus Mariupol
Mwanamke akipita mbele ya vifaru vya waasi wa Ukraine mjini DonetskPicha: Alexei Alexandrov/AP/picture alliance

Urusi kwa sasa imeelekeza mashambulizi yake katika kuliteka eneo la mashariki la Donbas ambalo lina mikoa miwili, Luhansk na Donetsk, mikoa ambayo kwa kiasi fulani iko chini ya udhibiti wa waasi wanaotaka kujitenga na wanaoungwa mkono na Urusi. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema majeshi yake ya hewani yameziharibu ndege sita zisizo na rubani za Ukraine mjini Luhansk.

Nalo jeshi la Ukraine Alhamis limesema limefanikiwa kuzuia mashambulizi 11 ya Urusi, likaharibu ndege nne na zaidi ya dazeni ya magari ya kijeshi ya Urusi vikiwemo vifaru. Mapambano yamefanyika pia kaskazini mashariki mwa mji wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, Kharkiv, ambapo utawala wa eneo hilo umesema mabomu ya Urusi yamesababisha kifo cha mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 11.

Chanzo: Reuters/AFP/DPA