1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matukio ya ukatili wa kijinsia yaongezeka Tanzania

24 Januari 2022

Matukio ya mauaji na ukatili wa kijinsia hasa kwa wanandoa yameendelea kuongezeka nchini Tanzania hali iliyoibua sintofahamu kuhusu usalama, hali ya afya ya akili na usimamizi wa haki za binadamu nchini Tanzania

https://p.dw.com/p/4614X
Afrika Liberia Entführung
Picha: Evelyn Kpadeh/DW

Matukio ya hivi karibuni ni pamoja na lile la  Januari 19, ambapo Shukrani Kamwela mwenye umri wa miaka 16, mkazi wa Ileje mkoani Songwe alimuua kwa kumchoma kisu mke wake aitwaye Subira Kibona mwenye umri wa miaka16 aliyekuwa ni mjamzito.  Tukio jingine ni lile la Desemba 27, la mwalimu wa Sekondari mkoani Singida, Simon Roman aliyefariki  baada ya kuchomwa moto na mkewe sababu ikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.

Akizungumzia matukio hayo msemaji wa Jeshi la Polisi nchini SACP Kamanda David Msime ambaye amesema licha ya ukubwa wake, lakini ni vigumu kwa matukio hayo kuzuiwa na doria za  kawaida za Jeshi la Polisi. Kadhalika amesema Jeshi hilo linaendelea kuchukua hatua kali kwa wanaofanya matukio hayo ikiwamo usimamizi wa kesi hizo kwa umakini ili adhabu zitolewe kwa mujibu wa sheria na kwa wakati.  Kamanda Misime anaelezea hapa ukubwa wa tatizo hilo nchini.

Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2021 watu 1 5 131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia huku ripoti hiyo ikionyesha ongezeko la mauaji kwa wanawake walio katika ndoa.

Ripoti  iliyotolewa  Septemba 2021 na Jarida la Afrika kuhusu hali ya ukatili wa kijinsia Tanzania miongoni mwa wanandoa, imeonyesha kuwa, asilimia 46 ya wanandoa hufanyiwa ukatili wa kijinsia, ambapo  asilimia 36 walifanyiwa ukatili wa kimwili na asilimia 32 walifanyiwa ukatili wa kisaikolojia na  asilimia 13 walifanyiwa ukatili wa kingono.

Mwandishi: Florence Majani DW Dar es Salaam