1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matokeo yaanza kutangazwa uchaguzi wa Nigeria

27 Februari 2023

Tume ya Uchaguzi nchini Nigeria (INEC) imeanza kutangaza matokeo ya majimbo kwa uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Jumapili, huku vyama vyote vikilalamikia mapungufu na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.

https://p.dw.com/p/4O16t
Mahmood Yakubu
Picha: Emmanuel Osodi/imago images

Matokeo ya kwanza kutoka jimbo la Ekiki yalionesha kura nyingi zilikwenda kwa mgombea urais wa chama tawala (APC), Bwana Bola Tinubu, ambaye alijikusanyia kura 200,000 dhidi ya Atiku Abubakar wa chama kikuu cha upinzani cha PDP aliyepata chini ya nusu ya kura hizo, huku Peter Obi wa chama cha Labour akipata kura 11,000.

Mara tu baada ya kutangaza matokeo hayo ya awali, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Mahmoud Yakubu, alisitisha kikao akisema kuwa kura zingeendelea kujumuishwa saa 5:00 asubuhi siku ya Jumatatu (Februari 27) kwa majira ya Nigeria.

Soma zaidi: Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Nigeria

Hata hivyo, vyama vyote vitatu vililalamikia kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi katika matukio kadhaa.

Mapungufu ya uchaguzi wa Jumapili

Nigeria | Schlange bei der Präsidentschaftswahl
Msongo wa wapigakura katika Chuo Kikuu cha Nnamdi Azikiwe nchini Nigeria.Picha: Patrick Meinhardt/AFP

Chama cha Labour, ambacho mgombea wake wa urais alitazamiwa kuonesha upinzani mkali kwa wagombea wa vyama viwili vikubwa, kiliikosowa vikali tume hiyo ya uchaguzi kwa kushindwa kuyapandisha matokeo kwenye tovuti yake kama ilivyoahidi kwa ajili ya kuhakikiwa. 

Zaidi ya masaa 24 tangu vituo kutakiwa kufungwa, vingi vyao vilikuwa bado havijayapandisha matokeo mtandaoni. 

Katika mkutano wao na waandishi wa habari, muungano wa asasi za kiraia nchini humo ulilalalamikia makosa na kushindwa kufunguliwa vituo kadhaa kwa wakati. 

Soma zaidi: Nigeria yaendelea na zoezi la kuhesabu kura

Tume ya Uchaguzi iliomba radhi kwa makosa hayo kupitia taarifa yake ikisema "... inafahamu changamoto zilizopo kwenye mfumo wake wa kuangalia matokeo, ambao umekuwa na kasi ndogo sana kutokana na hitilafu za kiufundi."

Vyama vya APC na PDP vililalamika kwamba maafisa wa tume ya uchaguzi walikuwa wakishinikizwa kuharibu matokeo kabla ya kuyawasilisha kunakohusika.

Matukio ya ghasia

Kuliripotiwa pia matukio ya ghasia na vitisho lakini sio kwa kiwango kilichoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita. 

Nigeria | Schlange bei der Präsidentschaftswahl
Wapigakura wakisubiri kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura jimbo la Yola, Nigeria.Picha: Sunday Alamba/AP Photo/picture alliance

Katika mkasa mmoja, wanajeshi waliingilia kati baada ya watu 15 waliojifanya maafisa wa tume ya uchaguzi kuvamia kituo cha kukusanyia matokeo katika kitongoji cha Alimosho, karibu na mji mkubwa wa kibiashara, Lagos, na kuwashambulia mawakala wa vyama kwa visu na magongo.

Soma zaidi: Nani atakuwa Rais mpya wa Nigeria?

Katibu wa chama cha Labour katika eneo hilo, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba wavamizi hao walimpiga kila mtu waliyemdhania kuwa mwanachama wa chama chake.

Hata hivyo, wanajeshi waliwatia nguvuni watu wote 15 waliohusika na tukio hilo.

Kura za urais na ubunge hukusanywa kwenye kila jimbo kati ya majimbo 36 ya Nigeria kabla ya hesabu zake kupelekwa kwenye kituo kikuu cha majumuisho katika mji mkuu, Abuja.

Vyanzo: Reuters, AFP