1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka wawili waachiwa huru na kundi la Hamas

Josephat Charo
24 Oktoba 2023

Kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas limewaachia huru mateka wawili ambao lilikuwa likiwauzilia. Mateka hao wamekabidhiwa kwa jeshi la Israel na wamepelekwa katika kituo cha afya.

https://p.dw.com/p/4Xvkt
Palestinian Hamas releases hostages
Mateka wawili, Nurit Cooper, anayefahamika pia kama Nurit Yitzhak na Yecheved Lifshitz baada ya kuachiwa na Hamas Oktoba 23.2023Picha: Al Qahera News/REUTERS

Shirika la msalaba mwekundu limethibitisha mateka wawili wameachiwa huru na kundi la Hamas na limewasafirisha nje ya Ukanda wa Gaza jana jioni. Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu imesema imesimamia kuachiwa huru kwa mateka hao na kwamba liko tayari kuendelea kufanya jukumu hilo katika siku za usoni.

Katika taarifa yake iliyotolewa hapo kabla, kundi la Hamas lilisema limewaachia huru wafungwa wawili wanawake kwa sababu za kibinadamu. Wanawake wawili wa Israel walioachiliwa na kundi hilo wamekabidhibiwa kwa jeshi la Israel na wamepelekwa katika kituo cha afya nchini Israel. Kwa mujibu wa taarifa ya afisi ya waziri mkuu wa Israel wanawake hao ni Nurit Cooper, mwenye umri wa miaka 79 na Yocheved Lifshitz wa umri wa miaka 85.

Israel imetaka kuachiliwa huru bila masharti mateka wote wanaoshikiliwa na kundi la Hamas ambalo linaorodheshwa kama la kigaidi na Israel, Umoja wa Ulaya, Marekani na mataifa mengine ya magharibi. Jeshi la Israel lilisema jana kwamba watu wapatao 222 walitekwa nyara na kupelekwa Gaza, wakiwemo raia wa kigeni.

Mwanamke mmoja Muisraeli, ambaye ni mama wa mateka wawili wanaozuiliwa na Hamas amesema hana taarifa yoyote kuhusu hali za watoto wake. Akizungumza na DW, Renana Gomeh, amesema mawasiliano ya mwisho aliyokuwa nayo na vijana wake kwa njia ya simu ilikuwa muda mfupi kabla kutekwa na Hamas na kupelekwa Gaza, na hajui waliko, au ikiwa wangali hai.

Borell ataka vita visitishwe kuruhusu misaada ya kibinadamu Gaza

Mwanadiplomasia mkuu wa Umoja wa Ulaya Josep Borell ametoa wito vita visitishwe katika Ukanda wa Gaza kwa sababu za kibinadamu. Akizungumza baada ya kukutana na mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg hapo jana, Borell amesema anaamini wazo la kusitisha vita kuratibu kuwasili kwa msaada wa kiutu, utakaowaruhusu watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kupata hifadhi, ni jambo ambalo viongozi wataliunga mkono.

Luxemburg | EU Außenministertreffen Josep Borrell
Josep Borell, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, (katikati) akiwasili kwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Luxembourg 23.10.2023.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Borell pia amesema hatua hiyo haipiti lengo la kuwa na kipindi cha utulivu kwa sababu za kibinadamu kilichoitishwa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Mawaziri kadhaa wa nchi za nje wa Umoja wa Ulaya wameitisha usitishaji wa vita kwa sababu za kibinadamu, huku mawaziri wengine, pamoja na Marekani na Israel, wakitoa kauli kupinga.

Hali ni tete katika hospitali za Gaza

Haya yanajiri huku hospitali za Gaza zikipungukiwa na mafuta ya jenereta. Mashirika ya habari yameripoti kwamba wodi mbili za watoto katika hospitali mbili katika Ukanda wa Gaza zina wasiwasi kuhusu kukosekana kwa umeme. Iyad Abu Zahar, mkurugenzi wa hospitali ya al-Aqsa katika mji wa Deir al-Balah katikati ya Ukanda wa Gaza ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba anahofia watoto kutoka wodi ya watoto huenda wakafa mara tu jenereta zitakapozima, akisisitiza kuwa jukumu walilonalo ni kubwa.

Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

Wafanyakazi wa kutoa misaada wamesema watoto wapatao 130 waliozaliwa mapema kabla wakati wao kufika wanakabiliwa na kitisho kikubwa katika vituo sita vya watoto. Ashraf al-Qidra, msemaji wa wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, amesema hospitali zinapungukiwa na mafuta na wanatumia mafuta kwa huduma muhimu pekee za kuokoa maisha, ikiwemo kuendeshea mashine za watoto waliozaliwa mapema kabla wakati, lakini hawafahamu wataendelea kufanya hivyo kwa muda gani.

Baerbock asisitiza umuhimu wa kupambana na Hamas

Wakati haya yakiarifiwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesisitiza umuhimu wa kupambana na ugaidi wa kundi la Hamas, ambalo limeorodheshwa kuwa la kigaidi nchini Ujerumani, Marekani na Umoja wa Ulaya. Katika kauli aliyoitoa kabla ziara yake kwenda New York, Marekani, Baerbock amesema haiwezekani kuwa na usalama wakati kukiwa na ugaidi wa Hamas, sio tu kwa Israel bali pia kwa Wapalestina.

Ameituhumu Hamas kwa kutaka kuchochea chuki katika jamii kote ulimwenguni, sio tu katika ulimwengu wa kiarabu. Amesisitiza kuwa msaada wa wakazi wa Gaza unatakiwa uendelee kutolewa kupitia kwa Umoja wa Mataifa na kutoa wito pawepo mazingira yatakayowawezesha wafanyakazi wa misaada wa umoja huo kutoa misaada katika Ukanda wa Gaza. Baerbock amesema suluhisho la mataifa mawili linaweza kuleta maisha ya amani baina ya Waisraeli na Wapalestina.