1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yatoa wito wa utulivu Jerusalem

8 Mei 2021

Mataifa kadhaa duniani yametoa wito wa kuwepo utulivu huku mengine yakilaani machafuko yanayoendelea kati ya Israel na Palestina ambayo yamesababisha zaidi ya watu 200 kujeruhiwa.

https://p.dw.com/p/3t8oS
Israel | Ausschreitungen in Jerusalem
Picha: Emmanuel Dunand/AFP/Getty Images

Miito imeongezeka leo Jumamosi ya kurejea kwa hali ya kawaida baada ya kuzuka makabiliano makali jana Ijumaa kwenye msikiti wa Al-Aqsa ambao ndio kitovu cha mvutano kati ya Israel na Palestina kwenye mji wa kale wa Jerusalem.

Saudia Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zimelaani mipango ya Israel ya kuwaondoa Wapalestina kutoka kwenye makaazi yao yaliyojengwa kwenye ardhi ambayo walowezi wakiyahudi wanadai kuimiliki.

Mipango hiyo ya Israel inafuatia usiku wa ghasia kwenye mji wa Jerusalem jana Ijumaa.

Polisi ya Israel ilifyetua risasi za mpira na maguruneti bandia wakiwalenga vijana waliokuwa wakivurumisha mawe kutoka msikiti wa Al-Aqsa.

Watu zaidi ya 200 wajeruhiwa katika vurugu

Israel | Ausschreitungen in Jerusalem
Picha: Ahmad Gharabli/AFP/Getty Images

Makabiliano hayo kwenye eneo la tatu kwa utakatifu katika dini ya Kiislamu na eneo jumla la Jerusalem Mashariki yamesababisha Wapalestina 205 kujeruhiwa pamoja na maafisa 17 wa polisi ya Israel.

Yametokea kutokana na ghadabu inayoongezeka juu ya mipango ya Israel ya kuwahamisha Wapalestina ili kutoa ardhi kwa walowezi wa kiyahudi.

"Saudi Arabia inapinga mipango yote ya Israel na hatua za kuwahamisha dazani ya Wapalestina kutoka kwenye nyumba zao huko Jerusalem ili kuanzisha utawala wake wa lazima" imesema sehemu ya taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya kigeni ya Saudia.

Umoja wa Falme za Kiarabu ambao mwaka uliopita ulirekebisha mahusiano yake na Israel "umelaani vikali" mapigano na mipango ya kuwahamisha Wapalestina na kuzirai mamlaka za Israel kupunguza mivutano.

Mapema siku ya Jumamosi raia kadhaa wa Israel wenye asili ya kiarabu waliandamana mjini Nazareth kuonesha mshikamano na Wapalestina kwenye mji wa Jerusalem wakibeba mabango yaliyosomeka "ukaliaji wa mabavu ni ugaidi"

Marekani na Umoja wa Ulaya nao walaani vurugu

Jerusalem | Sheik Jarrah | Demonstration
Picha: Tania Kraemer/DW

Marekani - mshirika wa karibu wa Israel - imesema inatiwa wasiwasi mkubwa na matukio yanayoendelea na kuzitolea wito pande mbili "kujiepusha na matendo yatakayochochea mivutano au kuvuruga amani"

"Hiyo inajumuisha mipango ya kuhamisha watu huko Jerusalem Mashariki, ujenzi wa makaazi ya walowezi, ubomoaji majengo na matendo ya kigaidi" imeongeza taarifa hiyo ya Marekani.

Umoja wa Ulaya kwa upande wake umezitaka mamlaka "kuchukua hatua za makusudi kupunguza misuguano ya sasa", ukisema "machafuko na uchochezi havikubaliki na wote wanahusika kutoka pande zote mbili ni sharti wawajibishwe"

Rais wa mamlaka ya ndani ya Palestina Mahmud Abbas amesema anailaumu serikali ya Israel kwa fujo zilizotokea na anawaunga mkono "mashujaa wa Al-Aqsa"