1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya G7 kujadili msaada zaidi kwa Ukraine

3 Novemba 2022

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizoimarika zaidi kiviwanda G7 wanakutana leo nchini Ujerumani kujadili namna ya kuratibu vyema msaada zaidi kwa Ukraine kufuatia mashambulizi katika miundombinu ya nishati.

https://p.dw.com/p/4J0Gt
Deutschland Münster | Vorbereitung auf G7-Treffen, Außenminister
Picha: Guido Kirchner/dpa/picture alliance

Viongozi hao kutoka mataifa ya Uingereza, Kanada, Ufaransa, Ujerumani,

Italia, Japan na Marekani watajumuika katika mkutano wa siku mbili katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Munster, na watajadili miongoni mwa mambo mengine, uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Ukuaji wa uchumi wa China na malengo yake kwa kisiwa cha Taiwan bila kuweka kando vitendo vya serikali ya Iran dhidi ya waandamanaji.

Zaidi sana viongozi hao wa mataifa saba ya kidemokrasia na yaliyoimarika zaidi kiviwanda, watatathmini hali nchini Ukraine karibu mwaka mmoja baada ya kukutana kwa mara ya kwanza walipoionya Urusi kwa "matokeo makubwa'' ikiwa ingeliendelea na mipango yake ya kuivamia Ukraine, jambo ambalo wakati huo wengine hakuamini kuwa lingeweza kutokea.

Soma zaidi:Viongozi wa G7 waazimia kukabiliana na kitisho cha njaa duniani 

Tangu onyo hilo kutolewa miezi miwili kabla ya uvamizi, mataifa ya G7 yametekeleza kwa kiasi kikubwa ahadi zao za kuiadhibu Urusi kwa kuiwekea vikwazo, ingawa hilo limeonekana kutoizuia Moscow, ambayo badala yake imeongeza mashambulizi yake na kuilenga miundombinu ya kiraia, imetuma askari zaidi, imenyakuwa kinyume cha sheria maeneo ya Ukraine na imekuwa ikitaja uwezekano wa kutumia silaha za kimkakati za nyuklia.

Umoja wa G7 dhidi ya uhaba wa chakula na nishati

Deutschland | G7 Gipfel | PK Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akizungumza na wanahabari katika mkutano wa G7: 28.06.2022Picha: Leonhard Foeger/REUTERS

Majadiliano hayo ya G7 yataangazia jinsi ya kukuza umoja wa nchi hizo katika

mzozo wa Ukraine, ambao umezidisha uhaba wa chakula na nishati duniani huku njaa ikizinyemelea sehemu kadhaa za Afrika na pia majira ya baridi kali yakikaribia barani Ulaya.

Mataifa ya Magharibi sasa yanatafakari jinsi ya kuweka kikomo kwenye bei ya uagizaji wa nishati ya Urusi kwa lengo la kuzuia zaidi mapato ya Kremlin katika matumaini kuwa hilo linaweza kuishawishi Urusi kukomesha uvamizi wake na kuelekea katika njia za kidiplomasia ili kuumaliza mzozo huo.

Soma zaidi: Urusi yaendeleza mashambulizi dhidi ya Ukraine

Wakati hayo yakiarifiwa, Urusi imeendeleza leo mashambulizi makali ya makombora katika miji kadhaa nchini Ukraine na hata katika kinu kikubwa zaidi cha nyuklia cha Zaporizhzhia ambacho kilizimwa kwenye gridi ya umeme ya taifa baada ya mitambo yake kuharibiwa na mashambulizi hayo.

Umoja wa Mataifa watupilia mbali azimio la Urusi

USA New York | Russland Blockiert UN Resolution
Viongozi wakijadili katika Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: ED JONES/AFP/Getty Images

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitupilia mbali hiyo jana jaribio la Urusi la kuanzisha tume ya kuchunguza madai yake yasiyo na msingi kwamba Ukraine na Marekani wanajihusisha na kile wanachokiita shughuli za " kijeshi za kibaolojia'' ambazo zinakiuka mkataba unaopiga marufuku matumizi ya silaha hizo.

Urusi ilipata tu kuungwa mkono na China katika kura ya azimio hilo huku Marekani, Uingereza na Ufaransa zikipiga kura ya "hapana" huku mataifa mengine 10 ya baraza hilo yakijizuia. Azimio hilo halikuidhinishwa kwa sababu haikuweza kupata kura tisa za "ndiyo'' zinazohitajika ili kupasishwa.