Mashirika ya ujasusi yahitaji mageuzi Ufaransa
6 Julai 2016Kamati hiyo ya bunge imesema Jumanne (05.07.2016) harakati za kupambana na ugaidi zinapaswa kuandaliwa upya kuwa chini ya asasi moja ya taifa na moja kwa moja kuwa chini ya mamlaka ya Waziri Mkuu.
Pia imependekeza hatua za kuimarisha ushirikiano kati ya polisi na vikosi vya kijeshi vya kuingilia kati pamoja na kuyaimarisha mashirika ya ujasusi.
Mkuu wa kamati hiyo ya wabunge Georges Fenech amesema hitimisho la repoti ya kamati hiyo imepitishwa kwa kauli moja na kwamba chombo kimeundwa kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yake.
Mashirika ya ujasusi yameshindwa
Amesema mashirika yao ya kijasusi yameshindwa na analitamka hilo bayana na kwamba hakuna mtu anayeweza kudanganya kwa hilo.
Fenech amesema "Lazima tapandishe sana kiwango cha kupambana na ugaidi wa kimataifa.Tunakabiliana na magaidi ambao wamefunzwa vyema katika masuala yote ya teknolojia ,wamefunzwa vyema katika mapambano na kufunzwa katika matumizi ya silaha.Katika kundi la Dola la Kiislamu kuna wanajeshi wengi wa zamani wa Iraq .Naweza kusema kwamba hatukabiliani na wahalifu wadogo wadogo."
Mwaka jana Ufaransa iikumbwa na mashambulizi ya risasi katika ofisi ya kijarida cha dhihaka cha Charlie Hebdo na duka la Wayahudi mjini Paris pamoja na shambulio katika ukumbi wa muziki wa Bataclan na jengine katika uwanja wa Stade de France hapo Novemba 13 ambalo limeuwa watu 130.
Mojawapo ya maeneo yaliyolengwa katika repoti hiyo lilikuwa ni suala la kuchunguzwa kwa watuhumiwa wa ugaidi.Wengi wa vijana wa kiume waliofanya mashmabulizi hayo hapo mwaka 2015 walikuwa wakijulikana na mashirika ya ujasusi ya Ufaransa wakimewa wachach waliowahi kutumikia vifungo gerezani na wakati fulani walikuwa wakifuatiliwa.
Asasi moja ya uchunguzi
Kamati hiyo ya uchunguzi ya bunge imependekeza kuwepo kwa asasi moja ya kupambana na ugaidi kufanana na ile ya Kituo cha Taifa cha Kupambana na ugaidi nchini Marekani ( NTC ) ambacho kiliundwa baada ya mashambulizi ya kigaidi nchini Marekani ya Septemba 11 mwaka 2001.Pia imetowa wito wa kuundwa kwa ofisi iliyojitolea ya ujasusi gerezani.
Kamati hiyo imeundwa kufuatia ombi la chama cha kihafidhina cha upinzani cha Republikan kuchunguza rasilmali zilizotolewa na taifa kupambana na ugaidi kufuatia mashambulizi ya Januari mwaka 2015.
Uchunguzi wa kamati hiyo pia umegunduwa kwamba hali ya hatari iliowekwa nchini humo kufuatia mashambulizi hayo na kumwagwa kwa maelfu ya wanajeshi kupiga doria mitaani imekuwa na taathira ndogo tu kwa usalama.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/dpa
Mhariri: Mohammed Khelef