1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW wataka UN kuiwekea vikwazo Myanmar

18 Septemba 2017

Mashirika ya haki za kibinaadamu yawahimiza viongozi wa dunia kuliwekea vikwazo jeshi la Myanmar linalodaiwa kuwafurusha Waislamu 400,000 wa jamii ya Rohingya katika kile kinachosemekana kuwa safisha safisha ya kikabila.

https://p.dw.com/p/2kBVg
Bangladesch Rohingyas im Flüchtlingslager Cox's Bazar
Picha: Reuters/M.P. Hossain

Wito huo kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binaadamu umetolewa huku Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likijitayarisha kukutana mjini New York, Marekani, na mgogoro wa Mnyanmar ukiwa moja ya masuala muhimu yatakayojadiliwa.

Kutimuliwa  kwa Waislamu wa jamii ya wachache ya Rohingya na kulazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh kumesababisha wito wa msaada wa dharura. Mashirika ya kutoa misaada hiyo yanajitahidi kutoa misaada kwa wakimbizi wapya wanaoingia, wengi wao wakiwa watoto. 

Hapo jana (Septemba 17), Myanmar ilisema haitaweza kuwarejesha wakimbizi wote waliokimbilia nchi jirani, ikiwashutumu baadhi yao wana mafungamano na wanamgambo wa Rohingya waliofanya mashambulizi mnamo Agosti dhidi ya vituo vya polisi na jeshi na ikawa sababu ya jeshi kuanza kuwashambulia. 

Kwa sasa, hatua yoyote ya kuwazuwiya wakimbizi kurejea Mnyanmar huenda ikasababisha Waziri Mkuu wa Bangladesh, Sheik Hasina, kulishinikiza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuiwekea shinikizo Mnyanmar kuwarejesha Warohingya wote walioko katika miji na makambi tofauti mpakani mwa nchi hizo mbili. 

HRW yataka warejeshwe kwa hiyari

Rohingya Krise in Bangladesch
Jamii ya Waislamu ya Rohingya wakiwa msituni kukimbia Mnyamar kuelekea Bangladesh.Picha: DW/M.M. Rahman

Wakati huo huo, shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch (HRW) limetoa wito kurejeshwa salama na kwa hiari kwa wakimbizi waliopoteza makaazi yao.

Shirika hilo pia limeuomba ulimwengu kuliadhibu jeshi la Mnyanmar kwa kuliwekea vikwazo kutokana na kile wanachodai ni maonevu yanayoendelea dhidi ya jamii ya wachache ya Rohingya.

Katika taarifa ya pamoja, HRW imelitolea wito Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuuweka mgogoro huu kuwa kipaumbele, kuhimiza mataifa kuweka marufuku ya kusafiri na kuzuwiya mali za maafisa wa Mnyanmar waliohusishwa na mateso, na pia kuweka vikwazo vya silaha.

Awali, jeshi la Myanmar liliwekewa vikwazo wakati wa utawala wake wa miaka 50, lakini baadhi ya vikwazo hivyo vimeondolewa katika miaka ya hivi karibuni baada ya majenerali kutoa nafasi ya mpito kuelekea demokrasia

Suu Kyi kuhutubia taifa

Huku hayo yakiarifiwa, kiongozi wa Mnyanmar, Aung San Suu Kyi, anajitayarisha kwa mara ya kwanza kutoa hotuba yake kupitia televisheni ya taifa kuzungumzia juu ya mgogoro unaoendelea.

Myanmar Aung San Suu Kyi in Wundwin
Kiongozi Mkuu wa Myanmar, Aung San Suu Kyi, anasema taarifa za mauaji dhidi ya Rohingya zinatiwa chumvi na mitandao ya habari.Picha: Reuters/S. Lewis

Suu Kyi, aliyewahi kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel, ameikasirisha jamii ya kimataifa kwa ukimya wake juu ya suala la Warohingya na pia kushindwa kulaani mambo yanayofanywa na jeshi ambalo anagawana nalo madaraka.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema hiii ni nafasi ya mwisho ya Suu Kyi kusimamisha janga la kibinaadamu linaloendelea. 

Kwengineko, serikali ya India imeiambia Mahakama ya Juu nchini humo kwamba baadhi ya Waislamu wa jamii ya Warohingya walioikimbia Mnyanmar ni kitisho kikubwa cha usalama, wakati ikitaka kuwarejesha makwao Warohingya 40,000 kutoka India.

Mukesh Mittal, afisa mkuu wa wizara ya sheria, amesema Mahakama ya Juu ni lazima iiridhie serikali kuchukua hatua kwa kuzingatia usalama wa nchi hiyo kufuatia baadhi ya Warohingya kuwa na rikodi ya misimamo mikali. 

Warohingya wamekanusha kuwa na mafungamano ya aina yoyote na makundi yaliyo na misimamo mikali.


Mwandishi: Amina Abubakar/AFP 
Mahriri: Yusuf Saumu