1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaharibu daraja jingine Severodonetsk

14 Juni 2022

Ukraine imesema daraja la tatu muhimu kwenye mji wa mashariki wa Severodonetsk limeharibiwa lakini mji huo bado unanafikika licha ya vikosi vya Urusi kuendelea kusonga mbele haraka kujaribu kuukamata.

https://p.dw.com/p/4CfmZ
Ukraine | Zerstörte Eisbahnbrücke in Raygorodok
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Mkuu wa utawala wa mji wa  Severodonetsk  ambao umekuwa kitovu cha mapambano makali kati ya vikosi vya Ukraine na Urusi amesema "shambulizi kubwa la kombora limeharibu daraja la tatu" linalokatisha mto Siverskyi Donets na kuunganisha mji huo na jimbo linalodhibitiwa na Ukraine la Lysychansk.

Afisa huyo Oleksandr Stryuk amekiambia kituo cha televisheni cha Ukraine kuwa licha ya hujuma hiyo nyingine mji wa Severodonetsk bado unafikika lakini kwa sehemu kubwa njia za mawasiliano zimeparaganyika. Amesema vikosi vya Ukraine vingali vinapambana "kuulinda mji huo" na kuna mapigano ya kila dakika na hali kwenye uwanja wa vita inabadilika haraka.

Hapo jana vikosi vya Ukraine vilisema vimewarejesha nyuma wanajeshi wa Urusi kutoka viunga vya mji wa Severodonetsk. Mkuu wa mji huo amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na jeshi la Urusi kuukamata kikamilifu mji wa Severodonetsk , wapiganaji wa Ukraine wamesimama imara kwenye uwanja wa vita.

Rais Zelenskyy ataka msaada zaidi wa silaha 

Hata hivyo Urusi na wapiganaji wa mashariki mwa Ukraine wanaoegemea Moscow wamesema kwa jumla wameuzingira mji huo wa viwanda na tangu jana ilisemekana njia zote muhimu za kuingia au kutoka Severodonetsk zimeharibiwa.

 Ukraine - Zustörung in Sievierodonetsk
Mapigano yamechacha kwenye mji wa SeverodonetskPicha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Inakadiriwa kuna karibu raia 540 hadi 560 ambao wamejificha kwenye kiwanda cha kemikali cha Azot katikati ya mji huo kuepuka mapigano yanayoendelea. Duru pia zimearifu kuwa ni vigumu kuwapatia msaada wowote raia hao kutokana na mapambano yanayoendelea.

Katika hotuba yake ya jana usiku rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksyy amezungumzia umuhimu wa kuvishinda vikosi vya Urusi kwenye maeneo yote ya nchi lakini amekiri kuwa jukumu hilo ni gumu.

Akizungumza kwa sauti ukakamavu Zelenskyy kwa mara nyingine alirejea wito wa kutaka nchi yake ipatiwe silaha zaidi kuvikabili vikosi vya Urusi.

"Gharama ya vita hii kwetu sisi ni kubwa sana. Inatisha. Na kila siku tunawatanabahisha washirika juu ya ukweli kwamba ni idadi ya kutosha ya silaha mamboleo ndiyo zitahakikisha Ukraine inapata upenyo na hatimaye kufikisha mwisho uonevu wa Urusi huko Donbas" amesema Zelenskyy 

Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la hospitali 

Ukraine-Krieg I Zerstörung in Soledar
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Katika hatua nyingine hapo jana watu watano waliuwawa kwa kombora kwenye mkoa wa mashariki mwa Ukraine wa Donetsk.

Kombora hilo liliilenga wodi ya wanawake wajawazito kwenye hospitali moja ya mkoa huo. Kila upande kwa maana ya Ukraine na Urusi zimelaumiana kuhusika na shambulizi hilo.

Kisa hicho kimezusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa Umoja wa Mataifa ambao umesema kuilenga miundombinu ya afya ni ukiukwaji usiovumilika wa sheria ya kimataifa.

Katika hatua nyingine Urusi imesema imeharibu shehena kubwa ya silaha na vifaa vya kijeshi vilivyopelewa Ukraine kutoka Marekani na mataifa ya Ulaya. Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema imehujumu pia kambi zinazotumiwa na wapiganaji mamluki nchini Ukraine.