1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano bado ni makali mjini Severodonetsk

Sylvia Mwehozi
13 Juni 2022

Jeshi la Ukraine limesema kuwa wanajeshi wake wamefurushwa katikati ya jiji la Severodonetsk, ambalo kwa wiki kadhaa limekuwa kitovu cha mashambulizi makali ya Urusi ya kudhibiti eneo la mkoa wa mashariki wa Donbas.

https://p.dw.com/p/4CcPD
Ukraine | Ukrainische Streitkräfte in der Stadt Sjewjerodonezk
Picha: ANATOLII STEPANOV/AFP

Vikosi vya Urusi vilishambulia kwa mizinga eneo la katikati mwa jiji hilo laSeverodonetsk na kuwafurusha wanajeshi wa Ukraine waliokuwa wamesalia. Taarifa ya jeshi la Ukraine, imesema licha ya hali hiyo, mapigano makali yameendelea kote katika mji huo na kwamba Ukraine bado inadhibiti karibu robo tatu ya mji wote.

Saa chache kabla, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema "kimsingi kila mita inapiganiwa" katika mji huo muhimu wa kiviwanda, ambako kamanda wa juu wa kijeshi alisema "ardhi imejaa damu". Katika hotuba yake kwa njia ya vidio Zelensky,  pia ameishutumu Urusi kwa kukishambulia kiwanda cha kemikali cha Azot katika mji wa Severodonetsk, ambako mamia ya raia wanaripotiwa kujificha. Lakini kiongozi wa jimbo la Luhansk ambalo linaungwa mkono na Urusi Leonid Pasechnik, aliwatupia lawama wanajeshi wa Ukraine kuwa ndio wanafanya mashambulizi kutokea ndani ya kiwanda hicho.

"Severodonetsk haijakombolewa kikamilifu kwa asilimia 100. Wanajeshi wa Ukraine, washiriki wa vita vya kitaifa wamesalia katika eneo la viwanda, kwenye kiwanda cha Azot ambako wanashambulia jiji," alisema Leonid.

Ukraine Zerstörung der Großstadt Sjewjerodonezk im Donbass
Jengo mjini Severodonetsk limeharibiwa na mashambuliziPicha: Alexander Reka/ITAR-TASS/IMAGO

Wakati huo, shirika la kimataifa la Amnesty International limeishutumu Urusi kwa uhalifu wa kivita nchini Ukraine, likisema kwamba mashambulizi katika mji wa Kharkiv, yamewaua mamilioni ya raia. Kwenye ripoti yake Amnesty international inadai kuwa "mashambulio ya mara kwa mara katika vitongoji vya makazi huko Kharkiv ni mashambulizi ya kiholela ambayo yaliua na kujeruhi mamia ya raia na hivyo ni uhalifu wa kivita."

Mbali na yanayoendelea kwenye uwanja wa mapambano, wajumbe wa shirika la kimataifa la biashara duniani WTO walikutana mjini Geneva siku ya Jumapili huku ajenda kubwa ikiwa ni namna ya kushughulikia kitisho cha ukosefu wa usalama wa chakula duniani kinachotokana na vita vya Ukraine. Kabla ya waziri wa uchumi wa Urusi kuzungumza katika mkutano huo, wajumbe kadhaa waliondoka ndani ya mkutano huo.Ukraine: Urusi inadhibiti asiliamia 70 ya Severodonetsk

Hayo yanajiri siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kusema kwamba Ukraine itafahamu ndani ya wiki moja juu ya hatma yake ya kujiunga na muungano huo.

Na ripoti iliyochapishwa hii leo inasema kuwa Urusi ilipata kiasi cha euro bilioni 93 kutokana na mauzo yake ya mafuta katika siku 100 za kwanza za vita vyake nchini Ukraine, na nyingi zilitumwa kwa Umoja wa Ulaya. Ripoti hiyo kutoka kituo huru chenye makao yake makuu nchini Finland cha utafiti wa nishati na hewa Safi (CREA) inatolewa wakati Kyiv ikizitaka nchi za Magharibi kusitisha biashara zote na Urusi kwa matumaini ya kuzuia mzunguko wa kifedha wa Kremlin.