1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua watu 18 Gaza

27 Agosti 2024

Watu 18 wakiwemo watoto wanane wameuawa kwa mashambulizi ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza usiku wa kiamkia Jumanne. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika mashambulizi hayo.

https://p.dw.com/p/4jxkv
Kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, Ukingo wa Magharibi
Kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, Ukingo wa MagharibiPicha: Majdi Mohammed/AP Photo/picture alliance

Maafisa wa Palestina wamesema kuwa watoto watatu na mama yao wameuawa katika shambulizi la anga la Jumatatu usiku kwenye kitongoji cha Tufah, kwenye mji wa Gaza, na watu wengine watatu hawajulikani walipo baada ya shambulizi hilo kutokea.

Wizara ya afya ya Gaza imesema kuwa shambulizi jengine la usiku limemuua mtoto mmoja, wanawake watatu na mwanaume mmoja huko Gaza.

Maeneo kadhaa yashambuliwa

Aidha, katika eneo la kusini mwa Gaza, watu watano wameuawa mapema Jumanne asubuhi katika shambulizi la Israel. Taarifa za maafisa wa hospital ya Nasser huko Khan Younis, imeeleza kuwa miongoni mwa waliouawa ni mwanaume mmoja na watoto wake watatu, na mwanamke mmoja.

Watu wengine watano wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi la anga kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi.

Jeshi la Israel limetangaza kuwa lililenga kushambulia eneo ambalo linatumiwa na wanamgambo wa Kipalestina kufanya shughuli zao katika kambi ya wakimbizi ya Nur Shams, na kwamba eneo hilo limeharibiwa.

Jengo likiwa limeharibiwa kwa mashambulizi ya Isral huko Khan Younis, Gaza
Jengo likiwa limeharibiwa kwa mashambulizi ya Isral huko Khan Younis, GazaPicha: Jehad Alshrafi/AP/picture alliance

Kulingana na taarifa za Palestina, droni ilifyatua makombora kadhaa dhidi ya kundi la watu wakati wa shambulizi hilo Jumatatu jioni. Ahmed Saleh Abdel Rahim, mkaazi katika kambi ya Nur Shams anaelezea jinsi mashambulizi hayo yalivyotokea.

"Saa nne usiku tulisikia firimbi ikipigwa, na ghafla shambulizi. Sekunde tano baadae mripuko mwingine ukasikika. Nilinyanyuka kuangalia kinachoendelea, na mripuko mwingine ukatokea. Hatukujua la kufanya, tuliogopa sana, sote tulitoka ndani ya nyumba," alifafanua Rahim.

Haijafahamika kama waliouawa ni raia au la

Hata hivyo, maafisa wa Palestina hawajasema iwapo waliouawa katika mashambulizi ya Israel ni raia au wapiganaji. Israel imekuwa ikisema inajaribu kutowadhuru raia na inaishutumu Hamas kwa kuwaweka raia hatarini kwa kupigana kwenye maeneo ya makaazi.

Wakati huo huo, Ikulu ya Marekani imesema mapigano makali kati ya Israel na Hezbollah mwishoni mwa juma hayakuvuruga mazungumzo ya kusitisha mapigano huko Gaza. Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani, John Kirby amewaambia waandishi habari Jumatatu usiku hapakuwa na atahri kwenye mazungumzo ya mjini Cairo.

Kirby amesema hatua ilipigwa wakati wa siku nne za mazungumzo ya ngazi ya juu ambayo yalikamilika bila kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda mrefu na kuachiliwa kwa mateka.

Wapalestina wakiondoka Deir al-Balah, Gaza baada ya Israel kutangaza amri ya kuondoka
Wapalestina wakiondoka Deir al-Balah, Gaza baada ya Israel kutangaza amri ya kuondoka Picha: Eyad Baba/AFPGetty Images

Katika hatua nyingine Umoja wa Mataifa umesema amri iliyotolewa mara 16 mwezi huu na jeshi la Israel kuondoka kwa wakaazi wa Gaza, kumesababisha Wapalestina kujibana kwenye maeneo madogo zaidi.

Hilo limechangiwa pia na kusitishwa kwa huduma za kituo cha kutoa misaada ya kiutu cha Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa Wapalestina, UNRWA bado linatoa huduma za afya na misaada mingine.

Hayo yanajiri wakati ambapo waziri wa Israel mwenye siasa kali za mrengo wa kulia, amesema atajenga sinagogi kwenye eneo la msikiti wa Al-Aqsa, huko Jerusalem matamshi ya uchochezi ambayo yameibua ghadhabu kubwa. Itamar Ben Gvir, Waziri wa Usalama wa Israel, amekiambia kito cha redio cha kijeshi kuwa iwapo itawezekana, atajenga sinagogi kwenye eneo hilo

(AFP, DPA, Reuters)