1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lasonga mbele kwenye maeneo ya Gaza

22 Agosti 2024

Vikosi vya Israel vimezidi kusonga mbele kwenye maeneo ya kati na kusini mwa Ukanda wa Gaza, ambapo wanapambana na wapiganaji wa Hamas, huku mashambulizi ya Israel yakiwaua takribani watu 22 katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4jm3J
Moshi ukionekana wakati wa mashambulizi ya Israel huko Deir el-Balah, Gaza
Moshi ukionekana wakati wa mashambulizi ya Israel huko Deir el-Balah, GazaPicha: Bashar Taleb/AFP

Maafisa wa afya wa Palestina wamesema kuwa katika mji wa kaskazini mwa Gaza, wa Beit Lahiya, shambulizi katika nyumba moja limewaua watu 11, huku shambulizi jengine likiwaua watu wengine sita, akiwemo mwandishi wa habari wa eneo hilo, katika nyumba moja kwenye kambi ya Al-Maghazi katikati mwa Ukanda wa Gaza. Watu wengine watano wameuawa kwenye mashambulizi tofauti, upande wa kusini mwa Gaza.

Jeshi la Israel limesema Alhamisi kuwa vikosi vyake vimeongeza operesheni zake kwenye mji wa Deir Al-Balah, katikati mwa Gaza na Khan Younis huko kusini, na kubomoa majengo kadhaa yanayotumika kijeshi, kugundua maroketi na kuwaua wanamgambo katika kipindi cha ndani ya saa 24 zilizopita. Jeshi hilo limesema vikosi vyake vimewaua wanamgambo 50 katika eneo la Rafah, kusini mwa Gaza siku moja iliyopita.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani, Joe Biden
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani, Joe Biden Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Mshambulizi hayo yanafanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kumshinikiza Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu udharura na umuhimu wa kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Ikulu ya Marekani imesema kuwa mazungumzo ya Biden na Netanyahu kwa njia ya simu Jumatano usiku, yamefanyika baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken, kumaliza ziara yake katika eneo la Mashariki ya Kati, ambayo haijaleta mafanikio katika vita vilivyodumu kwa miezi 10 sasa.

Madai ya Israel na Hamas yakwamisha makubaliano

Hamas inataka makubaliano yatakayositisha mapigano Gaza na kuachiwa wafungwa wa Israel na mateka wa kigeni huko Gaza, kwa kuachiliwa Wapalestina wengi waliofungwa katika magereza ya Israel. Hamas inaishutumu Israel na Marekani kwa kushindwa kufanikisha makubaliano hayo.

Netanyahu amesema vita vitamalizika tu Hamas itakaposhindwa, na kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kuruhusu kubadilishana mateka na wafungwa yatakuwa ya muda, huku kundi hilo la wanamgambo likiendelea kuwa kitisho.

Wapalestina wasio na makaazi wakiwa katika kambi ya Al-Maghazi, Gaza
Wapalestina wasio na makaazi wakiwa katika kambi ya Al-Maghazi, GazaPicha: Marwan Dawood/Xinhua/IMAGO

Wakati huo huo, afisa wa ngazi ya juu wa masuala ya kiutu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA Jonathan Whittall, amesema zaidi ya Wapalestina 100,000 walioyakimbia makaazi yao, wanahama tena baada ya jeshi la Israel kutoa amri mpya za kuwahamisha kwenye eneo lililofurika watu la Deir Al-Balah.

Kukosekana kwa mahitaji muhimu

Whittall amesema hawana mahitaji ya kutosha kuwapatia watu hao wanaoendelea kuhama.''Hatuna mahema ya kutosha kugawa kwa watu. Hatuna sabuni za kuwapa watu. Na usambazaji wa maji umepungua kwa asilimia 70, kwa sababu mitambo mingi ya kuondoa chumvi na visima vya maji viko ndani ya maeneo ambako watu wanatakiwa kuondoka. Kuna msongamano wa watu. Mazingira yaliyopo hayakubaliki,'' alisisitiza Whittall.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wasema misaada inashindwa kufika Gaza

Afisa huyo wa OCHA amebainisha kuwa hakuna sehemu ambayo ni salama Gaza wala sehemu ya kukimbilia kwa sababu watu hao wanazungukwa na mashambulizi ya anga na mizozo inayoendelea. Kulingana na Whittal, watu wana hofu kutokana na kuhamishwa kwa zaidi ya mara tano na wengine hadi 10, hali inayosababisha kuwepo kwa msongamano wa watu.

(AP, AFP, DPA, Reuters)