1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya Libya: Marekani mguu-nje, mguu-ndani

Admin.WagnerD22 Machi 2011

Marekani inataka ijitoe kwenye usimamizi wa mashambulizi dhidi ya Libya, mara tu baada ya awamu ya kwanza kumalizika, lakini vikosi vya Muungano wa Kimataifa vinapaswa kuhakikisha hatua hiyo inafanyika kwa usahihi.

https://p.dw.com/p/10f0k
Ndege ya jeshi la anga la Uingereza ikielekea Libya
Ndege ya jeshi la anga la Uingereza ikielekea LibyaPicha: AP

Rais Barack Obama anaonekana kusimamia kauli yake. Katika hotuba yake ya Juni 2009 mjini Cairo, Misri, alisema kwamba kwake yeye demokrasia, uhuru wa maoni, haki na sheria ndio msingi wa ustaarabu.

Lakini hili linaendana pia na msimamo wake mwengine kuwa, kila jamii inastahiki kujipatia mambo hayo kwa ufahamu na mwamko wake yenyewe, na hivyo: "Hakuna taifa linaloruhusika kuwalazimisha wengine mfumo wa utawala."

Kwa kusema hivi, Obama anajiwekea akiba ya maneno. Ulimwengu umechoka na tabia ya Marekani iliyokuwa ikioneshwa na mtangulizi wake, George Walker Bush, ambaye aliamini kuwa Iraq ilistahiki kushambuliwa kwa mabomu, ili ipate uelewa na uwezo wa kuwa na demokrasia ya kimagharibi.

Rais Barack Obama wa Marekani
Rais Barack Obama wa MarekaniPicha: AP

Kwa Obama hivi sasa, kujiingiza Libya kuna matokeo yake, na ndiyo maana amekuwa akichagua maneno ya kuielezea operesheni hiyo, kuwa ina lengo tu la kuwalinda raia na sio kubadilisha utawala.

Na tangu mwanzo Marekani iliweka wazi msimamo wake kuwa, sio tu hatua hii ilikuwa lazima iidhinishwe na Umoja wa Mataifa, bali pia iungwe mkono na Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu.

Ilikuwa ni Rais wa Ufaransa, Nikolas Sarkuzy, ambaye akiwa kwenye mji wake mkuu, alisimamia kikao cha kulifanyia kazi Azimio Namba 1973 la Umoja wa Mataifa dhidi ya Libya. Na ni ndege za Ufaransa ndizo zilizougotoa ufanyaji kazi wa operesheni hii.

Wawakilishi wa serikali ya Marekani wanasisitiza juu ya ushiriki wa mataifa mengi na mbalimbali katika Azimio hili na kwamba dhima ya Marekani isiwe kuongoza mashambulizi dhidi ya Libya wala kupeleka vikosi vya ardhini huko.

Kwa sura yoyote ile, Marekani inataka iendelee kucheza siasa za kilimwengu na wakati huo huo ikijitenga kando na matokeo yake.

Kwa sasa Marekani imejibebesha mzigo wa kutupa makombora yake na walikuwa ni makamanda wa Marekani waliopanga mashambulizi ya kwanza dhidi ya Libya.

Na hili haliendi mbali na balagha ya Rais Obama, ambaye anaonesha tu kuwa hakuna dola jengine ambalo linaweza kuipiku dhima ya Marekani. Na kwamba bila ya Marekani, hata huko NATO hakuna liwalo.

Serikali ya Marekani haiko tayari kuingiza mkono wake peke yake kutoa mkate kwenye tanuri. Lakini inachukuwa nafasi yake, si ziada wala pungufu ya hilo. Na dunia yapaswa kuuzoea ukweli huo!

Mwandishi: Christianne Bergmann/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Saumu Yussuf

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi