1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi dhidi ya Gaza yapamba moto

13 Novemba 2019

Watu 16 mpaka sasa wameuwawa Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya angani yanayofanywa na Israel dhidi ya wanamgambo wa Islamic Jihad,kundi ambalo linaungwa mkono na Iran.

https://p.dw.com/p/3SvNm
Israel Gaza Konflikt
Picha: picture-alliance/Photoshot/Jini

Mashambulizi yanayofanywa na Israel huko Gaza yameshasababisha watu 16 kuuwawa kufikia leo Jumatano. Wizara ya afya katika ukanda wa Gaza imesema Wapelestina wengine wanne wameuwawa leo kufuatia mashambulizi hayo.

Wapalestina hao wanne wameuwawa katika awamu mpya ya machafuko yaliyozuka jumanne asubuhi baada ya mashambulizi ya angani ya wanajeshi wa Israel kuilenga nyumba ya kamanda wa ngazi ya juu wa kundi la wanamgambo wa jihad na kumuua kamanda huyo pamoja na mkewe.

Kuanzia jana wapalestina 50 wengine wamejeruhiwa.Maafisa wa Ukanda wa Gaza wanasema mashambulizi mapya ya Israel yameshawauwa mpaka sasa wanamgambo wawili idadi ambayo pia imethibitishwa na kundi la wanamgambo wa kiislamu ambalo limesema wapiganaji wake wawili walishambuliwa katika wakati ambapo ufyetuaji roketi kuelekea upande wa Israel ukianza tena katika eneo la mpaka na Israel kulipiza kisasi  baada ya kushuhudiwa hali ya utulivu kiasi jumanne usiku.

Israel - Palästina - Konflikt l Raketenangriffe auf Israel
Picha: picture alliance/AA/A. Amra

Takriban wahanga wote wa mashambulizi ya Israeli ni wapiganaji wa kundi la Islamic jihad. Jeshi la Israel limesema kiasi roketi 220 kutoka Gaza zimefyetuliwa kuelekea Israel tangu Jumanne baada ya jeshi hilo kufanya mashambulizi upande wa Gaza na kumuua kamanda wa kundi hilo  ambaye inasemekana alikuwa ndie mpanga mikakati ya mashambulizi yote ya hivi karibuni dhidi ya Israel.

Kinachoshuhudiwa sasa katika eneo hilo tete la Mashariki ya kati ni mapigano makali ambayo hayajapata kutokea katika kipindi cha miezi kadhaa kati ya Israel na  kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran ambao wanatajwa kuwa watu wenye msimamo mkali zaidi kuliko hata watawala wa Gaza yaani kundi la Hamas.

Gaza Sprecher der Hamas Sami Abu Zuhri
Msemaji wa Hamas-Sami Abu ZuhriPicha: picture alliance/AA

Hata hivyo kundi la Hamas bado hadi sasa halijajiunga na mapigano hayo ishara ambayo inaonesha huenda ni mapigano ambayo hayatochukuwa muda mrefu. Juu ya hilo hali ya uchumi katika Gaza ni mbaya kiasi cha kwamba kundi la Hamas linaonesha halina hata hamu ya kuona duru nyingine ya mapigano.

Upande wa Israel shule zimeendelea kufungwa karibu na mpaka wa Gaza na watu pia wakiamrishwa kutokusanyika kwenye hadhara wakati roketi zikiendelea kuvurumishwa. Roketi zinazofyetuliwa kutoka Gaza  mpaka sasa zimefanikiwa kufika  mpaka kaskazini mwa mji wa Tel Aviv ambako watu wawili walijeruhiwa lakini hakuna kifo chochote kilichoripotiwa.

Israel ina mfumo wa ulinzi ambao kwa mujibu wa jeshi la Israel umefanikiwa kuzuia asilimia 90 ya roketi zinazorushwa kutoka Gaza. Pamoja na hali kuwa ya mashaka kutoka mjini Cairo, inaelezwa kwamba Misri ambayo mara nyingi inabeba dhima ya kuwa msuluhishi kati ya Israel  na wanamgambo wa Gaza inajaribu kuumaliza mvutano huo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW