Rais wa zamani wa Tunisia ahukumiwa miaka minane jela
24 Februari 2024Mahakama ya mjini Tunis imemhukumu rais wa zamani wa Tunisia Moncef Marzouki kifungo cha miaka minane jela baada ya kupatikana na hatia kwa kutaka kuchochea fujo.
Marzouki, ambaye alikuwa mkuu wa kwanza wa dola kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia baada ya vuguvugu la mapinduzi katika nchi za kiarabu la msimu wa machipuko mnamo mwaka 2011, anaishi nchini Ufaransa na hakuwepo mahakamani wakati hukumu hiyo ilipotolewa.
Msemaji wa mahakama amesema hukumu hiyo imetolewa kuzingatia kauli zilizotolewa na Marzouki zinazojumuisha uchochezi katika hotuba aliyoitoa mjini Paris.
Mnamo 2021 Marzouki alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela kwa kutishia usalama wa taifa baada ya kuitaka Ufaransa isitishe msaada wake kwa rais wa Tunisia Kais Saied kwenye maandamano ya mjini Paris.