1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiUfaransa

Marufuku ya Abaya imeibua ukosoaji Ufaransa

28 Agosti 2023

Wahafidhina wa Ufaransa wamepongeza uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku wanafunzi kuvaa Abaya, vazi linalovaliwa na baadhi ya wanawake wa kiislamu kama stara, hatua ambayo imeibua kauli za dhihaka na ukosoaji.

https://p.dw.com/p/4VfSb
Italien Ravenna | Symbolbild | Mädchen trägt Abaya Dress
Mwanamke aliyevalia vazi la Abaya ItaliaPicha: GoneWithTheWind/Imago Images

Ufaransa, ambayo iliweka marufuku kali kuhusu alama za kidini katika shule za serikali tangu karne ya 19 ambapo sheria ziliondoa ushawishi wa Kikatoliki kwenye mfumo wa elimu ya umma, imepata changamoto katika kuweka muongozo wa kukabiliana na jamii ya Kiislamu inayoongezeka.

Soma pia: Ufaransa yapania kupiga marufuku vazi la Abaya katika shule za umma

"Shule zetu zimeendelea kupitia majaribu kila wakati, na kwa kipindi cha miezi kadhaa kuna ongezeko la ukiukwaji wa  sheria ya msingi ya nchi ya kutoegemea dini, hasa kwa (wanafunzi) waliovalia mavazi ya kidini kama abaya na kameez au Sari,," Alisema Waziri wa Elimu Gabriel Attal siku ya Jumapili.

Sera na sheria ya msingi ya nchi kuhusu suala la dini, ambayo serikali ina jukumu kubwa zaidi katika kutenga mwonekano wa kidini kutoka kwa umma ni mada nyeti, na ambayo mara nyingi huchochea mvutano.

Soma pia: Mahakama ya Ulaya yaruhusu marufuku ya hijabu kazini

Mkuu wa chama cha kihafidhina cha Les Republicans, Eric Ciotti, alikuwa mwepesi kukaribisha hatua hiyo, akisisitiza kuwa chama chake kimekuwa kikiomba mara kwa mara kupigwa marufuku kwa vazi la Abaya.

Hata hivyo Clementine Autain, mbunge  kutoka chama cha  mrengo wa kushoto cha Insoumise, alikosoa hatua hiyo kwa kile alichokiita "polisi wa nguo" na kwamba ni hoja ya "tabia ya kupinga Waislamu".

Uwazi katika uamuzi

NO FLASH Kommission will Vollschleier aus Frankreich verbannen
Wanawake waliovalia niqab vazi la kufunika uso gubigubi UfaransaPicha: picture-alliance/dpa

Muungano wa wakuu wa shule wa SNPDEN-UNSA  kupitia katibu wa kitaifa Didier Georges, umekaribisha hoja, wakisema unachohitaji zaidi ya yote ni uwazi.

"Tulichotaka kutoka kwa mawaziri ni: ndio au hapana?" Georges alisema . "Tumeridhika kwa sababu uamuzi ulifanywa. Tungelikuwa na furaha vile vile iwapo uamuzi ungekuwa umeidhinisha Abaya.

"Tulikuwa na wasiwasi na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi wanaovaa Abaya. Na tunaamini kuwa haikuwa jukumu letu kusuluhisha, lakini jukumu la serikali," alisema Georges.

Soma pia: Maandamano ya kupinga marufuku ya Hijab Ufaransa

Mnamo 2020, mwalimu wa historia Samuel Paty aliuawa na mwanafunzi mwenye itikadi kali za kiislam katika shambulio ambalo liliibua maswali kuhusu maadili ya kidunia na jukumu la walimu.

Sophie Venetitay, kutoka muungano wa SNES-FSU, alisema ilikuwa muhimu kuzingatia mazungumzo na wanafunzi na familia ili kuhakikisha marufuku hiyo haikuwa na maana kwamba watoto wataondolewa kutoka shule za serikali kwenda shule za kidini.

Mnamo 2004, Ufaransa ilipiga marufuku hijabu shuleni na kufaulu pia kuweka marufuku ya niqab vazi la kufunika uso gubigubi hadharani mwaka wa 2010, na kuwakasirisha baadhi ya watu katika Jamii ya iliyo na Waislamu milioni tano.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Waziri wa elimu wa Ufaransa Gabriel Attal kusema mamlaka itapiga marufuku wanafunzi kuvaa Abaya wanapokuwa shule.

Katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa la TF1, waziri huyo ameeleza kuwa atafanya mazungumzo mapema wiki hii na wakuu wa shule za umma ili kuwasaidia kutekeleza marufuku hiyo.

Marufuku hiyo inatarajiwa kuanza kutekelezwa pindi tu muhula mpya wa shule utakapoanza mnamo Jumatatu ijayo.

Ufaransa imepiga marufuku mavazi au alama zozote za kidini katika shule za umma ikisema inafanya hivyo ili kutenganisha serikali na dini.

 

Vyanzo : Reuters//dpa