1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yapiga marufuku kampuni za China kwa kukiuka haki

8 Oktoba 2019

Marekani imesema itazipiga marufuku kampuni 28 za China kwa madai kwamba zinakiuka haki za bindaamu na kuwanyanyasa watu wa kabila la Uighur na Waislamu wa jamii nyingine za wachache kwenye jimbo la Xinjiang.

https://p.dw.com/p/3Qs6e
China Überwachungskameras in Xianjiang
Picha: Getty Images/AFP/P. Parks

Hata hivyo, Marekani imekanusha kuwa hatua hiyo inahusiana na mazungumzo ya biashara yaliyopangwa kuanza tena wiki ijayo.

Waziri wa Biashara wa Marekani, Wilbur Ross ameitangaza hatua hiyo akisema kwamba nchi yake haiwezi kuvumilia ukandamizaji na vitendo vya kikatili dhidi ya jamii ya walio wachache nchini China. Ross amesema kuwa marufuku hiyo itazizuia kampuni hizo kununua bidhaa za Marekani.

Miongoni mwa mashirika 28 yaliyoorodheshwa ni pamoja na ofisi 18 za usalama zilizoko Xinjiang, chuo kimoja cha polisi na kampuni nane za kibiashara, ikiwemo kampuni ya bidhaa za kiteknolojia ya Hikvision, pamoja na kampuni zinazoshughulika na vifaa vya ujasusi na kutambua sura ya mtu za Megvii na Sense Time.

Marufuku katikati ya mvutano

Marufuku hiyo imetangazwa huku kukiwa na mvutano kati ya Marekani na China, hasa kuhusu sera ya biashara na vitendo vinavyofanywa na China kwenye jimbo la magharibi la Xinjiang. Nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa duniani ziko katika vita ya kibiashara, ambapo zimekuwa zikiwekeana ushuru wa mabilioni ya dola kwenye bidhaa zake.

Jana, Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa mazungumzo kati ya nchi hizo mbili yamepangwa kuanza tena siku ya Alhamisi, huku mjumbe wa ngazi ya juu wa China katika masuala ya biashara, Liu He akitarajiwa kukutana na mwakilishi wa kibiashara wa Marekani, Robert Lighthizer na Waziri wa Fedha, Steven Mnuchin.

China Überwachungskameras in Xianjiang
Raia wa China akipita chini ya kamera za kutambua sura ya mtuPicha: Getty Images/AFP/G. Baker

Wakati huo huo, Marekani imechukua hatua zaidi dhidi ya China kutokana na sera zake kuelekea kwenye jimbo la Xinjiang. Mashirika ya kutetea haki za binaadamu yanasema kuwa China inawashikilia karibu Waighur milioni moja na Waislamu wengine katika kambi za ndani, ambako wanafundishwa propaganda za Kikomunisti na kulazimishwa kuukana utamaduni na dini yao, kitendo ambacho Marekani inasema ni sawa na enzi za utawala wa Wanazi nchini Ujerumani.

Madhila ya Waighur

Wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliandaa mkutano kuelezea madhila wanayopitia Waighur, huku Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Sullivan akiilani kampeni ya ukandamizaji ya China ambayo ni ya kutisha.

Sullivan alisema kuwa serikali ya China inawazuia Waislamu kusali na kusoma Quran na pia imeivunja au kuiharibu misikiti kadhaa. Amebainisha kuwa huo ni mfumo unaotumiwa na Chama cha Kikomunisti cha China kuwazuia raia wake kutekeleza haki yao ya uhuru wa kidini.

Hata hivyo, hadi hivi karibuni China imeyakanusha madai ya kuwepo kwa kambi hizo, lakini sasa imesema kuna shule za mafunzo ya ufundi, ambazo ni muhimu katika kudhibiti ugaidi, huku ikilalamikia kitendo cha kuingiliwa kwa masuala yake ya ndani.

(AFP, DPA, Reuters)