1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawaweka wanajeshi 8,500 tayari, mzozo wa Ukraine

25 Januari 2022

Wizara ya Ulinzi ya Marekani imewaamuru wanajeshi 8,500 kuwa tayari kwa uwezekano wa kupelekwa Ulaya kama sehemu ya wanajeshi wa NATO huku wakati wasiwasi ukizidi kuongezeka kuwa huenda Urusi itaivamia Ukraine.

https://p.dw.com/p/462Yl
USA Russland Ukraine | Konflikt | Pentagon-Sprecher John Kirby
Picha: Manuel Balce Ceneta/AP Photo/picture alliance

Kwa Marekani kuwaweka wanajeshi wake tayari kutumwa Ulaya, kunaashiria kudidimia kwa matumaini kwamba rais wa Urusi Vladimir Putin ataachana na kile ambacho rais wa Marekani Joe Biden amesema ni kitisho cha kuivamia Ukraine

Rais wa Marekani Joe Biden alishauriana na washirika wake wakuu wa mataifa ya Ulaya na kuwahakikishia ushirikiano wa Marekani katika juhudi za kusuluhisha na kujibu uvamizi wowote wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Urusi: Marekani inachochea mzozo wa Ukraine

Sehemu ya wanajeshi wa Ukraine wakifanya mazoezi ya kijeshi mjini Kyiv, Ukraine Januari 22, 2022.
Sehemu ya wanajeshi wa Ukraine wakifanya mazoezi ya kijeshi mjini Kyiv, Ukraine Januari 22, 2022.Picha: Efrem Lukatsky/Efrem Lukatsky/picture alliance

Msemaji wa makao makuu ya jeshi la Marekani Pentagon, John Kirby, amesema wanajeshi 8,500 wameshauriwa kuwa ange, tayari kutumwa Ulaya kama sehemu ya wanajeshi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO, hatua inayolenga kuashiria ushirikiano wa kukabili uchokozi wowote wa Putin.

"Kama ambavyo rais amesema, hata tunapoyapa mazungumzo na diplomasia kipaumbele, ni lazima pia tuzidishe utayari wetu. Kwa kutmiza wajibu wetu kiusalama katika jumuiya ya NATO. Marekani imechukua hatua za kuimarisha utayari wa vikosi vyake nyumbani na ughaibuni. Kwa hivyo wamejiandaa kwa mengi ikiwemo kuisaidia NATO kujibu shambulizi lolote hali ikitokea," amesema Kirby.

Urusi ambayo imewarundika wanajeshi wake karibu na mpaka na Ukraine, imekana kupanga kuivamia Ukraine na kwamba madai ya nchi za magharibi ni njama tu za NATO kufunika mipango yake yenyewe ya uchokozi.

Juhudi za kidiplomasia katika siku za hivi karibuni zimeshindwa kuleta suluhisho huku kila upande ukichukua hatua zinazodokeza hofu kwamba vita vitatokea.
Juhudi za kidiplomasia katika siku za hivi karibuni zimeshindwa kuleta suluhisho huku kila upande ukichukua hatua zinazodokeza hofu kwamba vita vitatokea.Picha: AFP

Marekani, EU wajadili jibu la pamoja kwa Urusi kuhusu mzozo wa Ukraine

Biden alifanya mazungumzo kwa njia ya video na wakuu wa nchi za Ulaya kwa dakika 80 kuhusu mrundiko wa wanajeshi wa Urusi karibu na Ukraine pamoja na jibu wanaloweza kutoa ikiwa uvamizi utatekelezwa.

"Mkutano ulikuwa mzuri sana. Sote tumekubaliana na wakuu wa Ulaya. Tutazungumzia hilo baadaye. Ahsante,” amesema Biden.

Ikulu ya rais White House imesema viongozi wamesisitiza haja ya kupata suluhisho la kidiplomasia lakini pia wamejadili juhudi za kuzuia uchokozi zaidi wa Urusi ikiwemo kuiwekea vikazo zaidi kiuchumi.

Hapo jana wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliziamuru familia za maafisa wake wa ubalozini walioko Kyiv kuondoka nchini humo pamoja na wale maafisa ambao majukumu yao si ya msingi.

Sintofahamu yaendelea kugubika mazungumzo kuhusu Ukraine

Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine wakifanya mazoezi ya kijeshi eneo la Donetsk, Ukraine, Disemba 23, 2021.
Baadhi ya wanajeshi wa Ukraine wakifanya mazoezi ya kijeshi eneo la Donetsk, Ukraine, Disemba 23, 2021.Picha: Ukrainian Defense Ministry Press Service/AP Photo/picture alliance

Mzozo huo ukiendelea kutokota, hatua ya Ujerumani kutojiunga na wenzake katika NATO kutoa silaha kwa Ukraine imewaghadhabisha baadhi ya washirika wake ambao sasa wanauliza kujitolea kweli kwa Ujerumani kuipinga Urusi.

Mjadala huo uliibuka mwishoni mwa wiki kufuatia ripoti kwamba Ujerumani iliizuia Estonia kuwapa Ukraine mizinga yake ya zamani kuisaidia kujilinda dhidi ya wanajeshi wa Urusi karibu na mpaka wake.

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alisema kweny eukurasa wake wa Twitter kwamba hatua hiyo ya Ujerumani haiambatani na uhusiano wao pamoja na hali ya sasa ya kiusalama.

Lakini kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aliyezungumza na waandishi habari mjini Berlin alisema hakuna uamuzi ambao ulifanywa kuhusu mizinga huku akisisitiza kwamba nchi yake itasimama pamoja na washirika wake katika NATO na Umoja wa Ulaya kupinga uvamizi wowote wa Urusi ndani ya Ukraine.

(APE)