1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yawakamata washukiwa wa mauaji ya Jovenel Moise

15 Februari 2023

Maafisa nchini Marekani wamewakamata watu wengine wanne jana, kuhusiana na mauaji ya rais wa Haiti Jovenel Moise.

https://p.dw.com/p/4NUvP
Haiti Ermordung Präsident Moise Witwe First Lady Martine Moise
Picha: Joseph Odelyn/AP Photo/picture alliance

Washukiwa ni pamoja na mmiliki wa kampuni ya usalama wa eneo la Miami ambaye aliwalipa wanajeshi wa zamani wa Colombia kuyafanya mauaji hayo.

Waendesha mashitaka wamesema Arcangel Pretel Ortiz, Antonio Intriago, Walter Veintemilla na Frederick Bergmann, wameshitakiwa kwa kuhusika katika mauaji hayo ya Julai 7, 2021, yaliofanywa na kundi la Wakolombia waliofunzwa kijeshi ambao waliandikishwa na Wahaiti walioko Florida.

Hali ni ya kukata tamaa Haiti, UN yaambiwa

Kukamatwa kwa washukiwa hao kumeongeza kwa wengine saba walioshtakiwa tayari katika njama hiyo, wakiwemo wanne ambao walihamishwa kutoka Haiti hadi Marekani mwezi uliopita kusomewa mashtaka.

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, njama hiyo ilipangwa mara ya kwanza na Mmarekani mwenye asili ya Haiti Christian Sanon, mmoja wa watu wanne walioshtakiwa mwezi uliopita, ambaye inadaiwa alitaka kuwa rais wa Haiti kwa kuchochea uasi dhidi ya Moise.