1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Marekani yatishia vikwazo vipya nchini Sudan

5 Mei 2023

Rais wa Marekani Joe Biden amesema mzozo wa Sudan unapaswa kumalizika na ametishia kuweka vikwazo vipya dhidi ya wale wanaohusika na umwagaji damu nchini humo.

https://p.dw.com/p/4QvdA
Rais Joe Biden wa Marekani ametishia kuwawekea vikwazo wahusika wa mzozo wa Sudan na kutaka mapigano yamalizwe mara moja.
Mzozo wa nchini Sudan unatishia kuibua janga kubwa la kiutu, hii ikiwa ni kulingana na mashirika ya kimataifa ya misaada ya kiutu.Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Rais Joe Biden amesema mapigano yanayoendelea ni usaliti wa matakwa ya watu wa Sudan ya kupatikana kwa serikali ya kiraia na kipindi cha mpito cha kidemokrasia. Matamshi hayo yametolewa kutokana na kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku saba baada ya mashambulizi ya anga na makombora kushuhudiwa kwenye mji mkuu, Khartoum.

Biden aidha amezitaka pande zinazohusika kumaliza mapigano, katika wakati kukiripotiwa mapigano katika mji mkuu Khartoum yaliyoingia siku ya 20, jana Alhamisi.

Biden amesaini amri ya rais jana Alhamisi inayoongeza mamlaka ya kuwawekea vikwazo kwa wahusika wanaotishia amani, usalama na utulivu wa Sudan pamoja na kudhoofisha mchakato wa mpito kwa njia ya demokrasia. Hata hivyo taarifa ya Biden haikuwataja walengwa.

Amesema mapigano nchini Sudan ni janga na usaliti dhidi ya watu wa taifa hilo wanaotaka serikali ya kiraia na mabadilishano ya kidemokrasia na kusisitiza machafuko ni lazima yamalizwe. Mamia ya watu tayari wamekufa kwenye mapigano yaliyozuka Aprili 15 kati ya jeshi la serikali linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na aliyekuwa makamu wake Hamdan Daglo wa Vikosi vya Dharura, RSF.

Soma Zaidi:Guterres: Mzozo wa Sudan sharti uzuiwe kuvuka mpaka

Miongoni mwa raia wa Suda anayeondoka nchini humo akiwa na mwanaye kutokana na mapigano yanaeondelea Sudan.
Mzozo unaoendelea nchini Sudan umesababisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbia makazi yao na wengine kwenda mataifa jiraniPicha: Amr Nabil/AP Photo/picture alliance

Katika mji mkuu Khartoum, mapigano yaliendelea kushuhudiwa siku ya jana na kuvuruga kabisa juhudi za kufikisha misaada ya kiutu kwa watu waliokwama baada ya kila wakati pande zinazohasimiana kuvunja makubaliano tete ya kusitisha mapigano, lakini pia ikiwa ni siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kuonya kwamba watu wa Sudan wanakabiliwa na janga kubwa la kiutu.

Bidhaa za chakula zaripotiwa kuibiwa Sudan.

Huku hayo yakiendelea, taarifa kutoka Geneva zimesema mpango wa chakula ulimwenguni, WFP umeripoti upotevu wa bidhaa za vyakula zenye thamani ya kati ya dola milioni 13 n 14 zilizopaswa kupelekwa Sudan, tangu kulipozuka mapigano hayo.

Mkurugenzi wa WFP nchini humo Eddie Rowe alipozungumza na shirika la habari la Reuters amesema bado wanazifanyia kazi taarifa za kuibiwa kwa bidhaa hizo, huku akielezea kukithiri kwa wizi nchini humo. Amesema kila uchwao wanaarifiwa kuhusu wizi wa bidhaa hizo.

Rowe anatoa taarifa hizi siku moja baada ya mkuu wa huduma za kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths kutoa mwito kwa pande zinazozozana nchini Sudan kuhakikisha njia salama za kupitisha misaada ya kiutu pamoja na watoa misaada.

Katika hatua nyingine, kutoka Nairobi taarifa zinasema karibu watu 12,000 wamekimbilia katika mji wa mpakani na Ethiopia wa Metemma, tangu mapigano hayo yalipozuka, hii ikiwa ni kulingana na shirika la kimataifa la wahamiaji, IOM.

Zaidi ya watu 1,000 wamewasili hivi karibuni, ambao ni pamoja na raia wa Sudan, raia wa Ethiopia wanaorejea nyumbani na watu wengine kutoka mataifa zaidi ya 50.

IOM imesema inawasaidia wakimbizi kwa kuwasafirisha kutoka mpakani hadi katika mji wa Gondar ulio karibu na mpaka huo na wengine hadi Addis Ababa. Kulingana na IOM, wengi wao hawana chochote, na ni juu yao kuwasaidia katika vituo vya kusubiri.