1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Hamas walitumia hospitali kutekeleza operesheni

Sylvia Mwehozi
15 Novemba 2023

Ikulu ya Marekani White House imesema kwamba wanamgambo wa Kipalestina wana kituo cha udhibiti katika hospitali ya Al-Shifa huko Gaza, kauli inayounga mkono utetezi wa Israeli wa harakati za kijeshi kwenye kituo hicho.

https://p.dw.com/p/4Yob4
Hospitali ya Al Shifa, kitengo cha dharura
Watu wakiwa wamesimama nje ya kitengo cha wagonjwa wa dharura ya hospitali ya Al-Shifa katika Jiji la GazaPicha: Khader Al Zanoun/AFP

Msemaji wa mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani John Kirby akinukuu vyanzo vya kijasusi vya Marekani, alisema Hamas na kundi la wanamgambo la Islamic Jihad la Palestina, wanaendesha "kituo na kudhibiti mtandao mpana kutoka hospitali ya Al-Shifa huko Gaza City."

"Tunazo taarifa kwamba Hamas na kundi la Islamic Jihad la Palestina walitumia baadhi ya hospitali katika Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na hospitali ya Al-Shifa na mahandaki ya chini kuficha na kusaidia operesheni zake  za kijeshi na kuwashikilia mateka. Hamas na wanachama wa Islamic Jihad wanaendesha kamandi na kudhibiti mtandao huo kutoka Al-Shifa katika Jiji la Gaza. Wamehifadhi silaha huko na wako tayari kujibu operesheni ya jeshi la Israeli dhidi ya hospitali hiyo."

Soma kuhusu: Vifaru vya Israel vipo kwenye milango ya hospitali ya Gaza

Hospitali ya Al-Shifa, Gaza
Picha ya satelaiti inaonyesha hospitali ya Al-Shifa, wakati mzozo ukiendelea kati ya Israel na kundi la HamasPicha: Maxar Technologies/Handout/REUTERS

Kauli hiyo ya Ikulu ya Marekani, iliyoungwa mkono na wizara ya mambo ya nje na ile ya ulinzi ya Pentagon, inatolewa wakati shinikizo likiongezeka kwa Israel kutokana na kuizingira hospitali kubwa ya Al-Shifa, ambapo madaktari wanasema wagonjwa na watu wanaotafuta makazi wamekwama katika mazingira ya kutisha. Hamas imesema matamshi hayo ya Ikulu ya White House yanachochea 'mauaji' zaidi katika hospitali za Gaza. 

Umoja wa Mataifa unakadiria takribani watu 2,300, wakiwemo wagonjwa, wafanyakazi na raia waliohamishwa, wamekwama ndani ya kituo hicho na watashindwa kuondoka kutokana na mapigano makali yanayoendelea karibu na kituo hicho.

Nalo jeshi la Israel limedai kudhibiti jengo la bunge la Gaza na taasisi nyingine za serikali zinazoendeshwa na kundi la Hamas katika eneo hilo, wakati wanajeshi wake wakizidisha mashambulizi kwenye maeneo ya Wapalestina. 

Taarifa hiyo imeongezea kwamba "taasisi za serikali za shirika la kigaidi la Hamas" zimetumika kwa "malengo ya kijeshi" ikiwa ni pamoja na "mafunzo ya kujiandaa kwa shambulio dhidi ya Israeli" mnamo Oktoba 7. Hata hivyo Hamas imetupilia mbali taarifa za jeshi la Israel za udhibiti wa taasisi zake. Afisa mmoja mwandamizi ndani ya Hamas Bassem Naim, alisema kwamba hatua hiyo ilikuwa ni "jaribio la kusikitisha na la kutengeneza ushindi na udhibiti wa kifikra wa maeneo matupu au ambayo yalilengwa na kuharibiwa hapo awali." 

Kilio cha Waandishi Habari huko Gaza

Fuatilia habari hii: Ukingo wa Magharibi: Vurugu za Waisrael zaongezeka dhidi ya Wapalestina

Kando na yanayoendelea ndani ya Gaza, juhudi za kidiplomasia za kuutanzua mzozo huo nazo zinaendelea. Hapo jana Qatar ilitoa wito kwa Israel na Hamas kufikia makubaliano ya kuwaachia mateka, ikionya kwamba hali inayoendelea Gaza inazidi kuwa mbaya kila kukicha.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Doha, msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed bin Mohammed Al-Ansari alisema hali ya "kuzorota" huko Gaza inatatiza juhudi za upatanishi.

Aliongeza kuwa wanaamini hakuna nafasi nyingine kwa pande zote mbili zaidi ya upatanishi huo kufanyika na kufikia hali ambayo italeta mwanga wa matumaini katika mgogoro huo mbaya. Taifa hilo la Ghuba limeongoza mazungumzo ya kuachiliwa kwa mateka na usitishaji mapigano kwa muda sasa.

Ikumbukwe kuwa siku ya Jumatatu kundi la Hamas lilisema Israel imeomba kuachiliwa huru kwa wanawake 100 na watoto kwa mabadilishano ya watoto 200 wa Kipalestina na wanawake 75 wanaoshikiliwa katika jela za Israel.