1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Marekani yakubali kuisaidia Afghanistan

11 Oktoba 2021

Serikali mpya ya Taliban inasema Marekani imekubali kutoa msaada wa kibinaadamu kwa watu wenye uhitaji mkubwa, huku Marekani ikisema kuwa mazungumzo ya ana kwa ana baina yao yalikuwa ya kuambizana ukweli na ya kitaalamu.

https://p.dw.com/p/41WCK
Katar Doha Taliban
Picha: REUTERS

Kwa mujibu wa Taliban, mazungumzo hayo yaliyofanyika jana mjini Doha, Qatar, yalimalizika kwa Marekani kukubaliana na ombi la msaada kwa raia wanaoteseka kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, ingawa iliendelea kukataa kuutambua utawala wa Taliban. 

Marekani inasema maafisa wake na wa Taliban walikutana ana kwa ana ukiwa mkutano wa kwanza baina ya pande hizo mbili tangu Taliban kuchukuwa madaraka nchini Afghanistan, lakini maafisa wa Marekani waliweka wazi kwamba Taliban watahukumiwa kwa vitendo vyao na sio maneno matupu.

"Ujumbe wa Marekani ulijikita kwenye masuala ya usalama na wasiwasi wa ugaidi na pia njia salama ya kuwapitisha raia wa Marekani, wageni na washirika wetu wa Kiafghani wanaotaka kuondoka Afghanistan, na pia haki za binaadamu, ikiwemo ushiriki wa wanawake na wasichana kwenye nyanja zote za jamii ya Kifghani." Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Ned Price, alisema.

Msemaji wa masuala ya kisiasa wa Taliban, Suhail Shaheen, aliliambia shirika la habari la AP kwamba, waziri wa nje wa Afghanistan aliihakikishia Marekani kwenye mazungumzo hayo kwamba Taliban imejitolea kuona kwamba ardhi ya Afghanistan haitumiki na makundi ya siasa kali kufanya mashambulizi dhidi ya mataifa mengine.

Ukuruba wa tahadhari

Afghanistan | Simon Gass trifft Amir Khan Muttaqi
Mwakilishi maalum wa Uingereza kwa Afghanistan, Simon Gass (kushoto), akipeana mikono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan, Amir Khan Muttaqi.Picha: social media/REUTERS

Kauli za pande za mahasimu hao wawili zinaashiria kuanza upya kwa safari ya majadiliano kati yao, miaka 20 baada ya Marekani kuivamia Afghanistan na kuiangusha serikali ya Taliban, na kisha kuitumbukiza nchi hiyo kwenye janga la miongo miwili la mauaji, wakimbizi, na ufukara. 

Hata hivyo, kwa Marekani kukataa kuutambua utawala wa Taliban kisiasa, kunafanya masuala mengine ya kiusalama na kiutawala kushindikana baina yao. Juzi, Jumamosi, Taliban iliondosha kabisa uwezekano wa kushirikiana na Marekani katika mapambano dhidi ya kundi lijiitalo Dola la Kiislamu, ambalo limezidisha mashambulizi yake nchini Afghanistan, tangu kuondoka kwa majeshi ya kigeni yakiongozwa na Marekani.

Kundi hilo la IS ama Daesh, ambalo ni hasimu mkubwa wa Taliban, limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa, yakiwemo ya Ijumaa iliyopita kwenye msikiti mmoja wa Waislamu wa madhehebu ya Shia, ambayo yaliuawa watu 46.

Taliban inasema inao uwezo wa kukabiliana na kundi hilo bila msaada wa kigeni, huku Marekani ikiamini kuwa Daesh ndicho kitisho kikubwa cha kigaidi kwake kutokea nchini Afghanistan.

Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yamejikuta kwenye wakati mgumu wa kuchaguwa nchini Afghanistan. Yanajaribu kufikiria jinsi ya kushirikiana na Taliban kuwasaidia maelfu ya Waafghani wanaokabiliwa na hali ngumu ya kimaisha, bila ya kulipa kundi hilo uhalali wa kisiasa linaoutaka.