1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaidhinisha chanjo ya Pfizer kwa watoto wa miaka 12

11 Mei 2021

Mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani FDA imeidhinisha matumizi ya dharura ya chanjo dhidi ya virusi vya corona ya BioNTech-Pfizer kwa watoto kuanzia miaka 12 na kuendelea.

https://p.dw.com/p/3tDdy
BioNTech COVID-19 Impfstoff
Picha: Douglas R. Clifford/Tampa Bay Times/ZUMA/picture alliance

 

Dr. William Gruber, mtaalamu wa chanjo ya BioNTech/Pfizer na magonjwa ya watoto iliyoko Cincinatti nchini Marekani amesema "Leo tuna furaha kubwa kusikia kwamba FDA imepanua matumizi ya dharura ya chanjo ya BNT162 B2 kwa watoto wa miaka 12 hadi 15. Kwa hiyo huu ni wakati wa nafuu kubwa kwetu, kwa kuzingatia uwezo wetu wa kupambana na janga la COVID-19."

Chanjo ya BioNTech-Pfizer ni chanjo ya kwanza kuruhusiwa kutumika kwa watoto wa chini ya miaka 16 nchini Marekani.

Taarifa ya FDA imesema takriban visa milioni 1.5 vya maambukizi kwa watoto wa kati ya miaka 11 na 17 vimeripotiwa kwenye taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, CDC nchini humo tangu Aprili mwaka jana hadi Aprili 30 mwaka huu.

Mkurugenzi wa idara ya tathmini ya kibaiolojia na utafiti wa FDA Peter Marks ametoa hakikisho kuhusiana na ufanisi wa chanjo hiyo, akisema imethibitishwa kukidhi viwango vya kutumika kama dharura kwa watoto wa umri huo.

BioNTech-Pfizer na Moderna kwa pamoja zimeanza majaribio ya ufanisi wa chanjo kwa watoto wa hadi miezi sita hadi miaka 11.

Indien Bangalore | Coronavirus, Patient
Mgonjwa wa COVID-19 nchini India. Taifa hilo linakabiliwa na wimbi la pili la maambukizi, huku virusi vipya vikiibua wasiwasi zaidi.Picha: Abhishek Chinnappa/Getty Images

WHO yatangaza wasiwasi zaidi kufuatia kuibuka kwa virusi vinavyojibadilisha.

Huku hayo yakiendelea, shirika la afya ulimwenguni WHO, limetangaza kubadilisha uainishaji wake kwa virusi vya corona vinavyojibadilisha, aina ya B.1.617 vilivyogunduliwa nchini India, ambavyo sasa wanaviweka katika kundi la virusi vinavyoibua wasiwasi.

Tangazo hilo limetolewa na mwanasayansi mwandamizi wa WHO Maria van Kerkhove aliyesema zipo taarifa zinazoashiria kuongezeka kwa kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo nchini India.

Kulingana na shirika hilo, virusi vinavyotia wasiwasi ni vile vinavyochukuliwa kuwa hatari zaidi kuliko vile vilivyogundulika mwanzoni nchini China. Virusi vilivyogunduliwa Uingereza, Brazil na Afrika Kusini pia vimeendelea kuibua wasiwasi kwa shirika hilo.

Wataalamu wanahofia kwamba kuzidi kusambaa kwa virusi kunaongeza kitisho cha kuwa sugu dhidi ya chanjo.

Nchini Ujerumani, waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer ameambukizwa virusi vya corona, na kuwa waziri wa karibuni kukutwa na maambukizi, baada ya waziri wa afya Jens Spahn, aliyeambukizwa Oktoba mwaka jana.

Waziri huyo sasa amejitenga nyumbani kwake, ingawa hana dalili yoyote. Kulingana na shirika la habari la DPA, Seehofer alipata chanjo ya Pfizer-BioNTech mwezi uliopita.

Utoaji wa chanjo umeendelea nchini Ujerumani ambayo pia imeruhusu utoaji wa dozi moja ya chanjo ya Johnson & Johnson kwa watu wazima na kuondoa mfumo wa makundi ya vipaumbele kwa watu wanaopata chanjo, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa afya, Spahn.

Mashirika: DPAE/DW