1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Marekani yagundua 'uhalifu wa kivita' Ethiopia

21 Machi 2023

Marekani imehitimisha kuwa wanajeshi wa Ethiopia na Eritrea pamoja na waasi walifanya uhalifu wa kivita wakati wa vita vikali vilivyodumu kwa miaka miwili, kaskazini mwa Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4Oxpb
Tigray-Krise in Äthiopien
Picha: UGC/AP/picture alliance

Blinken, ambaye alisikika kuwa mwenye matumaini wakati akiwa nchini Ethiopia kuhusu uwezekano wa kupatikana amani baada ya muafaka wa Novemba 2, alitoa wito mkali wa uwajibikaji aliporejea Washington. Akizungumza wakati akizindua ripoti ya kila mwaka ya Marekani kuhusu haki za Binaadamu, Blinken alisema vitendo vingi vilivyofanywa havikuwa vya kubahatisha au matokeo tu ya kivita. Vilipangwa na kufanywa makusudi. "Baada ya wizara ya mambo ya kigeni kuchunguza kwa umakini sheria na ukweli, nimehitimisha kuwa vikosi vya Ulinzi wa Kitaifa vya Ethiopia, Vikosi vya Ulinzi wa Eritrea, vikosi vya TPLF na vikosi vya Amhara vilifanya uhalifu wa kivita wakati wa vita vya kaskazini mwa Ethiopia."

Äthiopien Friedensabkommen Tigray
Serikali na waasi wa TPLF walisaini makubaliano ya amaniPicha: PHILL MAGAKOE/AFP/Getty Images

Blinken aliongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Kigeni pia iligundua kuwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu ulifanywa na vikosi vya Ethiopia, Eritrea na Amhara, ikiwemo mauaji na unyanyasaji wa kingono, ijapokuwa hakutaja TPLF.

Soma pia: Ethiopia yatoa onyo juu ya uchunguzi wa vita vya Kaskazini

Vikosi vya kikanda vya Amhara vilipigana Pamoja na serikali. Blinken alisema vilifanya kile alichokiita usafishaji wa kikabila kwa kuwahamisha kwa nguvu watu kutoka magharibi mwa Tigray. Amezihimiza serikali ya Ethiopia na serikali ya Eritrea Pamoja na TPLF kuwawajibisha wale waliohusika na ukatili huo.

Soma pia: Marekani na Ethiopia wajadili uwajibikaji huko Tigray

Blinken pia alizungumzia uwajibikaji wakati wa ziara yake mjini Addis Ababa, ambako alifanya mkutano mrefu usio wa kawaida na Waziri Mkuu Abiy Ahmed na kuzungumza pia na kiongozi wa TPLF Getachew Reda. Lakini hakutaja moja kwa moja uhalifu wa kivita au uhalifu dhidi ya ubinaadamu wakati akiwa Addis Ababa.

Blinken akutana na viongozi wa Ethiopia

Waziri huyo wa mambo ya kigeni amesema ameona kutoka kwa pande zote nchini Ethiopia dhamira ya kurejesha amani ikiwemo kuwajibishwa waliohusika na vita. "Hali tunayoona sasa nchini Ethiopia ni tofauti sana na hali katika maeneo mengine ya ulimwengu kwa sababu kwa miezi minne ilyopita, hatua ambazo pande zote zimechukua kutekeleza makubaliano ya kusitisha uhasama zimeokoa maisha na kuyabadilisha maisha ya makumi ya maelfu, mamia ya maelfu ya watu."

Abiy alikuwa ameelezea hasira wakati Blinken wakati wa vita hivyo alizungumza kwa jumla kuhusu uhalifu dhidi ya ubinaadamu na kiongozi hiyo wa Ethiopia amepinga juhudi za uchunguzi zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Blinken alipoulizwa kuhusu muda wa kutolewa kwa matokeo ya uchunguzi huo, alisema ilifaa kutoa tathmini hiyo katika wakati wa uzinduzi wa ripoti ya haki za binaadamu. 

Soma pia: Waasi wa Tigray waanza kuzisalimisha silaha zao nzito

Marekani katika siku za nyuma ilikadiria kuwa karibu watu 500,000 waliuawa katika mgogoro huo wa miaka miwili, na kuufanywa kuwa mojawapo ya vita vikali Zaidi vya karne ya 21 na hata kuipiku kwa mbali idadi ya vifo kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Ripoti hiyo ya kila mwaka iliibua upya wasiwasi wa Marekani kuhusu haki za binaadamu katika nchi kadhaa ulimwenguni ambazo mara kwa mara hushutumiwa. 

afp, reuters