1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaendelea kuongoza maambukizi ya COVID-19

31 Machi 2020

Idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa COVID-19 nchini Marekani imepindukia 3,000, kwa mujibu wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, huku walioambukizwa wakizidi 163,000 na bado hali inahofiwa itazidi kuwa mbaya.

https://p.dw.com/p/3aEDA
USA Donald Trump PK Coronavirus
Picha: Getty Images/W. McNamee

Takwimu zilizotolewa na chuo hicho kufikia jioni ya jana zinaonesha kuwa vifo 3,008 vimetokea, na watu 163,429 wameambukizwa, hiki kikiwa kiwango cha juu kabisa cha maambukizi kushinda hata Italia, Uhispania na China.

Rais Donald Trump amekosolewa vikali kwa kuchelewa kuchukuwa hatua madhubuti mwanzoni mwa kuenea kwa kirusi hicho nchini mwake.

Picha za kuogofya kutoka hospitali za jiji la New York na kwengineko kote Marekani, zimeibuwa ukweli kwamba mfumo wa afya nchini humo haukuwa umetayarishwa kwa mapambano haya, kwani kuna uhaba mkubwa wa vifaa vya kawaida kama vile maski na mashine za kupumulia.

Siku ya Jumapili, Trump alifuta mipango yake ya kufuta muda wa watu kujitenga mnamo tarehe 12 Aprili na kuongeza hadi mwishoni mwa mwezi, baada ya wanasayansi wa ngazi za juu kumkabili wakiwa na takwimu zinazoonesha kupanda kwa maambukizi.

Trump amesema huenda idadi ya vifo ikafikia hadi 200,000 kabla ya kirusi hicho kudhibitiwa.

China yarikodi maambukizi mapya

China | Coronavirus | Rückkehr zur Normalität
Licha ya kutangaza kwamba kimsingi imeushinda ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi cha corona, China inasema ina wagonjwa wengine 48 wapya.Picha: Getty Images/AFP/H. Retamal

Nayo China, licha ya kutangaza kwamba kimsingi imeushinda ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na kirusi cha corona, sasa imethibitisha wagonjwa wengine 48 wapya, kutoka 31 waliokuwa nao siku moja kabla.

Kamisheni ya Afya ya nchi hiyo imesema wagonjwa wote 48 wamepatikana China Bara, na walikuwa wametokea nje ya nchi hiyo.

Kufikia siku ya Jumatatu, watu waliogundulika kuambukizwa kirusi cha corona walikuwa 771, ingawa Kamisheni hiyo ya Afya imesema kuwa hakuna maambukizi mapya ya ndani hadi sasa.

Kwa siku nne mfululizo, China ilikuwa haina rikodi ya mgonjwa yeyote mpya.

Katika taifa jirani la Korea Kusini, idadi ya maambukizi mapya hivi leo ni 125, ambayo inafanya watu waliokwishapatwa na ugonjwa huo kufikia 9,786.

Na huko Mexico, taifa la Amerika Kusini, wizara ya afya imesema watu 1,094 wameshaambukizwa kirusi hicho kufikia jana, huku 28 wakipoteza maisha yao.

Rais wa zamani wa Kongo afariki kwa COVID-19
 

Brazzaville Hauptstadt der Republik Kongo
Sanamu la rais wa zamani wa Kongo, Jacques Joaquim Yhombi Opango, kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Brazaville.Picha: Getty Images/AFP/Junior D. Kannah

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kongo, Jacques Joaquim Yhombi Opango, amefariki dunia kwa kirusi cha corona nchini Ufaransa, akiwa na umri wa miaka 81.

Mtoto wake, Jean-Jacques, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba baba yake alifariki dunia kwenye hospitali moja mjini Paris hapo jana kwa ugonjwa wa COVID-19.

Kwa mujibu wa mtoto wake huyo, Yhombi Opango, aliyeitawala Kongo kuanzia mwaka 1977 hadi alipopinduliwa mwaka 1979, tyari alikuwa mgonjwa kabla ya kuambukizwa kirusi hicho.

Afisa huyo wa zamani wa jeshi alizaliwa mwaka 1939 katika jimbo la kaskazini mwa Kongo la Cuvette, na aliingia madarakani baada ya kuuawa kwa Rais Marien Ngouabi, kabla ya mwenyewe kupinduliwa na kiongozi wa muda mrefu, Denis Sassou Nguesso.

Alifungwa jela kutoka mwaka 1987 hadi 1990, akituhumiwa kushiriki jaribio la kutaka kumpindua Sassou Nguesso, na alipoachiliwa alianzisha chama cha kisiasa lakini akashindwa uchaguzi mwaka 1992.

Baadaye aliungana na Rais Pascal Lissouba na kuwa waziri wake mkuu baina ya 1994 na 1996. Mwaka 1997 alikimbilia Ufaransa baada ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na akarejea miaka kumi baadaye, mwaka 2007.