1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaanza mchakato wa kujiondoa katika WHO

8 Julai 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ameanzisha rasmi mchakato wa kuiondoa Marekani katika shirika la afya duniani WHO na kutimiza kitisho chake cha kusitisha ufadhili kwa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3ewxm
South Dakota, Keystone I Donald Trump am Mount Rushmore National Memorial
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Wanaharakati wa afya ya umma pamoja na wapinzani wa kisiasa wa Trump, wameelezea kutoridhika kwao na hatua ya kujiondoa kwa Marekani katika shirika hilo la afya duniani WHO linaloongoza mapambano dhidi ya ugonjwa wa kupooza, surua na afya ya akili kote duniani pamoja na janga la virusi vya corona katika wakati ambapo visa vya maambukizi ya virusi hivyo vimekuwa vikiongezeka kote duniani.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, amesema kuwa baada ya kutishia kusimamisha ufadhili wa dola milioni 400 za mchango wa kila mwaka wa Marekani kwa shirika hilo na baadaye kutangaza kujiondoa kwa taifa hilo katika shirika hilo, serikali ya Trump imetuma taarifa rasmi kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Muda wa kujiondoa kwa Marekani katika shirika la WHO

Mchakato wa Mwanzilishi huyo mkuu wa shirika la WHO kujiondoa katika uanachama wa shirika hilo utachukuwa muda wa mwaka mmoja kufikia Julai 6 mwaka 2021.

Huku hayo yakijiri, bara Afrika sasa limethibitisha zaidi ya nusu milioni ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo na vituo vya Afrika vya kuzuia na kudhibiti magonjwa, bara hilo lina visa laki tano na 80 elfu vya maambukizi baada ya Afrika Kusini kurekodi visa zaidi ya elfu 10 kwa siku moja, likiwa ndiyo taifa lenye maambukizi zaidi.Hata hivyo wiki iliyopita, mkuu wa shirika la WHO barani Afrika Matshidiso Moeti, alisema kuwa idadi kamili ya visa vya maambukizi barani Afrika haijulikani kwasababu mataifa yake 54 yanakabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa vya kupima virusi hivyo.

Makundi ya uhalifu yatoa bidhaa duni katika mapambano dhidi ya virusi vya corona

Wakati huo huo, Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu na mihadarati UNODC imesema kuwa makundi yaliojipanga ya wahalifu wanaotumia hofu na hali ya kutoeleweka inayozingira janga la virusi vya corona, yanatoa bidhaa duni kushughulikia ongezeko la mahitaji ya bidhaa muhimu za kukabiliana na virusi hivyo na pengo lililoko katika kupata bidhaa hizo.

Katika taarifa, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Ghada Waly, amesema kuwa afya na maisha ya watu yamo hatarini huku wahalifu wakitumia vibaya mzozo wa ugonjwa wa COVID-19 kujipatia pesa kutokana na hofu ya umma na ongezeko la mahitaji ya bidhaa za kinga ya kibinafsi na dawa. Shirika hilo limetoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa na mifumo ya kisheria ikiwa ni pamoja na faini na mafunzo zaidi kwa wale wanaofanya kazi katika sekta ya matibabu na kusema hiyo ndio njia ya pekee itakayowezesha ufanisi wa hatua za kukabiliana na virusi hivyo.