1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zashutumiana katika Umoja wa Mataifa

Oumilkheir Hamidou
23 Agosti 2019

Baada ya kubatilishwa mkataba wa kutotengeneza silaha za nuklea, Urusi inasema Marekani inajiandaa kujirundukia silaha." Marekani nayo inasema haitaki "kupakata mikono" wakati Moscow inaendelea kujiimarisha kijeshi.

https://p.dw.com/p/3OMmY
DW Karikatur - INF-Vertrag offiziell beendet
Picha: DW/Sergey Elkin

Wawakilishi wa Urusi na Marekani wamekaripiana katika kikao cha Umoja wa Mataifa jana, kila mmoja akimshutumu mwenzake kuanzisha mbio za kutengeneza silaha, huku China ikisema haitojihusisha na makubaliano ya aina yoyote ya makombora.

Mapema mwezi huu, Marekani na Urusi walibatilisha makubaliano yaliyotiwa saini Disemba nane mwaka 1987 ya kutotengeneza makombora ya nuklea yanayoweza kushambulia hadi umbali wa kilomita 5420-makubaliano yaliyofikiwa katika enzi za vita baridi, baada ya kila upande kuulaumu wa pili kuyaendeya kinyume makubaliano hayo.

Urusi imependekeza kuitishwa kikao cha baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baada ya Marekani kufanya jaribio la nuklea na kufyetua kombora la masafa ya wastani mapema wiki hii-kombora hilo ni miongoni mwa yale ambayo yamepigwa marufuku kufanyiwa majaribio.

Jaribio la kombora la masafa ya wastani la Marekani
Jaribio la kombora la masafa ya wastani la MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/Scott Howe/The Defense Department of the US

China yakataa kujumuishwa katika maalumbano ya mbio za silaha

Naibu balozi wa Urusi katika umoja wa Mataifa, Dimitri Polyansky amekosoa kile alichokiita "unafiki wa Marekani" na kusisitiza kwamba "Marekani imefanya makusudi kuvunja makubaliano ya INF na kwamba jaribio la kombora lililofanaywa Agosti 18 ni ushahidi wa hali hiyo."

Polyanski ameliambia pia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba jaribio hilo limedhihirisha "Marekani iko tayari kwa mashindano ya kurundika silaha" katika wakati ambapo Urusi ilikuwa tayari kwaajili ya mazungumzo kuhusu namna ya kudhibiti silaha.

Akijibu hoja hizo ,mwenzake wa Marekani Jonathan Cohen amesema Urusi imeamua kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita, kuvunja masharti ya makubaliano ya INF na imetega makombora kadhaa ya nchi kavu yenye uwezo wa kushambulia vituo katika nchi za Ulaya."

Cohen amesema pia kwamba Urusi na China " bado wangependelea kuwa na ulimwengu ambako Marekani itakuwa ikijizuwia huku wao wakiendelea kutengeneza silaha bila ya shida.

Cohen amehoji badala yake pawepo mkataba mpya wa kudhibiti silaha utakaoijumuisha pia China.

Lakini balozi wa China katika Umoja wa Mataifa Zhang Jun amejibu akisema viongozi wa mjini Beijing "hawaoni umuhimu wowote wa kujiunga na makubaliano kama hayo.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dw.com

Mhariri: Grace Patricia Kabogo