1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zajadili mkataba kuhusu zana za nyuklia

John Juma Mhariri: Iddi Ssessanga
22 Juni 2020

Wajumbe wa Marekani na Urusi wanajadiliana mjini Vienna kuhusu mkataba wa silaha za nyuklia, wakati ambapo mvutano ukiongezeka iwapo mataifa hayo mawili yanaona thamani yoyote katika kudhibiti umiliki wa silaha.

https://p.dw.com/p/3eA3j
Berlin Protest gegen Auflösung des INF-Vertrages
Picha: Imago Images/epd/C. Ditsch

Rais wa Marekani Donald Trump anashikilia kuwa China inapaswa kushirikishwa kwenye mazungumzo hayo kuhusu makubaliano ya New Start ambayo ni ya kudhibiti umiliki wa vichwa vya nyuklia baina ya Marekani na Urusi, akidai hadi sasa, China imekuwa na uhuru wa kufanya itakavyo kutengeneza mifumo ya silaha.

China kwa upande wake imeonyesha kutokuwa na nia ya kujiunga kwenye mazungumzo hayo, na hivyo kuzusha lawama kutoka Marekani. Hata hivyo wachambuzi wanahoji kuwa Marekani inauona msimamo wa China kama fimbo muhimu ya kukabiliana na uhasama unaoendelea kukua dhidi yake.

Ujumbe kwenye mazungumzo hayo haukutoa taarifa yoyote ulipowasili mapema leo katika ukumbi wa mkutano Vienna, mji mkuu wa Australia.

SIPRI: Nchi zenye silaha za nyuklia zaendelea kuziimarisha

Mjumbe maalum wa Marekani katika mazungumzo hayo Marshall Billingslea alituma picha kwenye ukurasa wa Twitter ikionyesha viti vitupu na bendera ya China kwenye mazungumzo hayo, pamoja na maelezo kuwa China haipo kwenye mazungumzo. Hatua ambayo imeshutumiwa na China ikisema hawakuwa wamepanga kushiriki mazungumzo hayo.

Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Ryabkov akiwasili katika ukumbi wa mazungumzo kuhusu mkataba wa New START mjini Vienna
Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Ryabkov akiwasili katika ukumbi wa mazungumzo kuhusu mkataba wa New START mjini ViennaPicha: picture-alliance/A. Demcisin

Billingslea ameongeza kwamba China ingali inajificha nyuma ya ukuta mkubwa wa siri kuhusu utengenezaji wake wa silaha za nyuklia na mambo mengine mengi. Hata hivyo tutaendelea na Urusi.

Daryl Kimball ambaye ni mkurugenzi mkuu wa chama cha kudhibiti umiliki wa zana za kivita, chenye makao yake makuu mjini Washington, amesema msisitizo wa kuishirikisha China kwenye mazungumzo hayo unaonyesha utawala wa Trump hauzingatii kikamilifu utekelezwaji wa mkataba huo.

Soma pia: Kim Jong Un aitisha kikao cha dharura kuelekea muda wa mwisho wa mazungumzo ya nyuklia

Tayari Rais Trump amefuta mikataba kadhaa na Urusi, mathalan kuhusu makombora yenye nyuklia angani pamoja na makombora ya masafa ya wastani.

Wasiwasi waongezeka kuhusu mustakabali wa mkataba wa kudhibiti nyuklia ulimwenguni

Wasiwasi waongezeka kuhusu mustakabali w amkataba unaodhibiti umiliki wa zana za nyuklia kati ya Marekani na Urusi
Wasiwasi waongezeka kuhusu mustakabali w amkataba unaodhibiti umiliki wa zana za nyuklia kati ya Marekani na UrusiPicha: picture-alliance/dpa/TASS/V. Ivashchenko

Licha ya hayo yote, Marshall Billingslea pamoja na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergei Ryabkov wanatarajiwa kujadili mustakabali wa mkataba huo uliosainiwa mwaka 2010 na ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2021.

Muda huo ni mchache sana kusaini upya mkataba huo, na hata kukubaliana kuhusu mkataba mpya utakaojumuisha China, hasa ikizingatiwa uchaguzi wa Marekani umekaribia mwezi Novemba.

Marekani na Urusi zinakadiriwa kumiliki takriban asilimia 90 ya silaha za nyuklia ulimwenguni.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kumalizika kesho Jumanne.

Vyanzo: DPAE, AFPE, RTRE