Marekani na China zakwaruzana
12 Desemba 2016Msemaji wa wizara ya masuala ya nchi za kigeni wa China Geng Shuang amesema kuwa iwapo sera hiyo ya China Moja inayotoa muongozo wa uhusiano kati ya serikali ya Beijing na eneo lenyE mamlaka yake ya ndani la Taiwan itabatilishwa ama kutatizwa, uhusiano kati ya China na Marekani pamoja na ushirikiano wa sekta mbali mbali kati ya mataifa hayo mawili utakuwa jambo gumu kutekeleza.
Serikali ya China inalichukulia eneo la Taiwan kuwa muhimu sana katika uhuru wake na ulinzi wa mipaka yake na kuongeza kuwa uzingatiaji wa sera hiyo ya China Moja ndicho kigezo cha kisiasa katika uhusiano wake na Marekani.
Shuang aliongeza kuwa matamshi hayo ya Trump wakati wa mahojiano kupitia runinga mwishoni mwa juma, yanatishia kusambaratisha uhusiano kati ya Marekani na China.
Lakini kulingana na Trump, haoni sababu ya kuzingatia sera hiyo ya China moja iwapo hawatakubaliana na China kuhusiana na masuala mbali mbali ikiwemo biashara. Aliilaumu China kwa kuiumiza Marekani na pia kutetea vikali hatua ya kuwasiliana kwa njia ya simu na Tsai Ing-Wen, rais wa eneo lenye mamlaka yake ya ndani kidemokrasia la Taiwan mapema mwezi huu, eneo ambalo halijadhibtiwa na Beijing kwa zaidi ya miaka 60.
Ijapokuwa Marekani ni mshirika mkuu wa Taiwan na msambazaji wake wa silaha, Marekani haijakuwa na uhusiano rasmi wa kidiplomasia na eneo hilo tangu mwaka 1976 ilipoanza kuitambua Beijing.
Mwandishi: Tatu Karema
Mhariri:Yusuf Saumu