1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuteua balozi wake nchini Sudan

Admin.WagnerD5 Desemba 2019

Baada ya miaka 23 ya mahusiano yaliyopwaya, Marekani imetangaza kuwa itateua balozi wake wa nchini Sudan wakati ikimkaribisha mjini Washington kiongozi mpya wa kiraia wa taifa hilo la kaskazini mashariki ya Afrika. 

https://p.dw.com/p/3UG41
USA Abgeordneter Eliot Engel mit Regierungschef der Übergangsregierung in Sudan Abdullah Hamduk
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok (Kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Bunge la Marekani.Picha: AFP/J. Watson

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo ametangaza mpango wa nchi yake wa kumteua balozi mpya mjini Khartoum baada ya kuridhishwa na kile Marekani imekitaja kuwa juhudi zinazofanywa na waziri mkuu mpya wa mpito nchini Sudan  Abdalla Hamdok.

Hamdok ambaye amekuwa mjini Washington kwa ziara ya kikazi anakuwa kiongozi wa kwanza wa Sudan kuitembelea Marekani tangu mwaka 1985.

Marekani imesifu hatua za mapema ambazo Hamdok amezichukua kuachana na sera na mwenendo wa utawala uliopita ambao ulituhumiwa na serikali ya mjini Washington kwa kuwa na mahusiano na makundi ya itikadi kali pamoja na sera katili dhidi ya raia nchini Sudan.

Jina la balozi litasubiri idhini ya Seneti 

USA Präsident Donald Trump und Mike Pompeo
Picha: AFP/B. Smialowski

Pompeo amesema balozi mpya wa Marekani atatangazwa baada ya kuidhinishwa na Baraza la Seneti huku Sudan nayo itarejesha uwakilishi wake wa kibalozi  mjini Washington.

"Hii ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha mahusiano baina ya mataifa yetu mawili" ameandikia Pompeo kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Pompeo amemsifu  Hamdok kwa kuonesha nia ya kufanya mazungumzo ya kusaka amani na makundi ya upinzani,  kuanzisha tume ya kuchunguza ukatili uliofanywa dhidi ya waandamanaji pamoja na mipango ya kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia baada ya kukamilika miezi 39 ya kipindi cha mpito.

Akiwa mjini Washington, Hamdok amekutana na kufanya mazungumzo na maafisa kadhaa wa Marekani ingawa hakupangiwa kukutana na Pompeo wala rais Donald Trump ambao wote wawili walikuwa nje ya nchi kwa ziara za kikazi.

Hamdok alichukua madaraka nchini Sudan mnamo mwezi Agosti baada ya miezi kadhaa ya maandamano yaliyoongozwa na vijana yaliyofanikiwa kumng`oa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir na baadaye Baraza la Kijeshi lililojaribu kusalia madarakani.

Maandamano hayo yalichochewa na hasira za kupanda kwa gharama za chakula na changamoto nyingine lukuki za kiuchumi.

Udhaifu wa mahusiano kati ya Khartoum na Washington 

Unruhen im Sudan | Demonstration
Picha: picture-alliance/Photoshot

Marekani ilikuwa na mahusiano dhaifu na AlBashir aliyechukua hatamu za uongozi mwaka 1989 na kukumbatia siasa zinazoegemea dini ya kiislam ikiwa ni pamoja na kumkaribisha nchini humo aliyekuwa kiongozi wa kundi la Al- Qaeda, Osama bin Laden.

Suala jingi lillotia doa uhusiano baina ya mataifa hayo mawili, ni uamuzi wa Marekani wa kuiweka Sudan kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi, kitu ambacho serikali mpya ya Hamdok inakitaja kuwa kizingiti kwenye kuvutia uwekezaji kutoka nje.

Mvutano uliongeza zaidi kufutia ukandamizaji wa Al Bashir kwenye jimbo la magharibi la Darfur katika kampeni ya kijeshi ambayo Umoja wa Mataifa unaitaja kuwa mauaji ya halaiki na kutaka kiongozi huyo wa zamani kufunguliwa mashtaka.

Mwezi uliopita waziri mkuu Hamdok alilitembelea eneo la Darfur na kukutana na mamia ya wahanga na kuwahakikishia anafanyia kazi matakwa ya kupatikana kwa amani ya kudumu.