1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kusitisha oparesheni kwenye gati la misaada Gaza

Hawa Bihoga
15 Juni 2024

Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani CENTCOM imesema hali mbaya ya hewa katika bahari imesababisha kusitishwa kwa muda oparesheni katika gati la kupitishia misaada ya kibinadamu kuingia eneo la Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4h4uP
Haki za Binadamu | Mlinzi na mbwa wakikagua midaada inayopelekwa Gaza.
Mlinzi akiwa na mbwa wakikagua misaada kabla ya kuruhusiwa kuingia katika eneo la Ukanda wa Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

CENTCOM, imesema hayo kupitia chapisho lake katika mtandao wa X na kuongeza kwamba gati hilo litaelekezwa katika bandari ya kusini mwa Israel ya Ashdod, na uamuzi huo umechukuliwa ili kuzuia uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na kuchafuka kwa bahari, pia ili liweze kuendeleza kutoa huduma zaidi katika siku za usoni.

Soma pia:Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza

Taarifa ya Kamandi hiyo imeongeza kwamba gati hilo litarejeshwa katika ufuo wa Gaza mara tu hali ya hewa itakapotengemaa.

Bandari hiyo ya muda inatumika kama kitovu cha utoaji wa misaada inayohitajika Gaza na tangu Mei 17 zaidi ya tani 3,500 zimewasilishwa kupitia eneo hilo.