1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Marekani: Israel imruhusu Mkuu wa UNRWA kuingia Gaza

Hawa Bihoga
20 Machi 2024

Marekani imesema Israel inapaswa kumruhusu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA kuingia Gaza, baada ya Israel kumzuia kutokana na kile ilichokisema hakufuata utaratibu.

https://p.dw.com/p/4dux6
Israel, Jerusalem | Mkuu wa UNRWA Philippe Lazzarini
Mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini akiwa katika mkutano na waandishi wa hababri.Picha: Mostafa Alkharouf/Anadolu/picture alliance

Marekani ambae ni mshirika wa karibu wa serikali ya Israel imetoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja baada ya mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini, kulalamika kuwa Israel ilimzua kutembelea Gaza ambayo imeharibiwa vibaya na vita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Marekani Vedant Patel amesema, imani yao ni UNRWA iweze kufanikiwa kutembelea eneo la oparesheni, na kwamba wataendelea kushirikiana na serikali ya Israel ili kuidhinisha vibali vya wafanyazi wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada.

Soma pia:UN: Nusu ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na baa la njaa

Aidha Patel ameongeza kuwa "Serikali zote za kikanda zinahitaji kufanya kile kinachohitajika kuwezesha mwitikio wa kibinadamu, ikienda sanjari na kuruhusu uingiaji huru wa wafanyakazi wa kimataifa."

Hakuzungumzia zaidi iwapo Marekani imeweza kuzungumzia hilo moja kwa moja na mamlaka ya Israelx, ili kufanikisha uingiaji wa wafanyakazi wa kimataifa.

Israel: Lazzarini hakufuata utaratibu

Wizara ya ulinzi ya Israel inayosimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina inayokaliwa kwa mabavuCOGAT, ilisema siku ya Jumatatu kwamba Lazzarini hakufuata "michakato na njia muhimu za uratibu" wakati wa kuomba kuingia Gaza.

"Hili ni jaribio lingine la UNRWA la kulaumu Israeli kwa makosa yao wenyewe," COGAT iliandika kwenye mtandao wake wa X, ambao zamani ilijulikana Twitter.

Umoja wa Mataifa | Mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini
Mkuu wa shirika la UNRWA Philippe Lazzarini akiwa nje ya ofisi za Umoja wa MataifaPicha: Johanna Geron/REUTERS

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, aliwaambia waandishi wa habari kwamba shirika hilo "halijapokea kile walichifikiri kuwa ni maelezo halali" kwa kunyimwa kuingia Gaza.

Israel imeshutumu kuwa wafanyakazi wa UNRWA takriban 13,000 wa Gaza walihusika katika shambulio la Oktoba 7, ambalo lilichochea kampeni ya kijeshi ya Israel katika ukanda huo, na kulishutumu shirika hilo kwa kuwa mstari wa mbele kwa Hamas.

Soma pia:Mkuu wa shirika UNHCR ataka ufadhili wa UNRWA urejeshwe tena

Marekani na wafadhili wengine kadhaa walisimamisha ufadhili kwa UNRWA kupisha uchunguzi, hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken ameitaja kazi ya shirika hilo kuwa ya thamani kubwa.

UNRWA wiki iliyopita ilisema shambulizi la Israel lilipiga moja ya vituo vyake vilivyosalia vya usambazaji wa chakula katika Ukanda wa Gaza, huku Israel ikisema kuwa ilimuua mwanamgambo wa Hamas.

Mashambulizi ya ardhini yatatatiza juhudi za upatanishi

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema bado amedhamiria kutekeleza mashambulizi ya ardhini katika eneo la Rafah, licha ya mashaka ya Rais wa Marekani Joe Biden.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Hapo awali, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Qatar Majed al-Ansari alisema kuwa "wana matumaini makubwa" baada ya mazungumzo ya Doha na Mkuu wa kijasusi wa Israel yaliyolenga kujaribu kufikia usitishaji mapigano.

"Operesheni ya ardhini ya Israeli, katika eneo la Rafah kungerudisha nyuma mazungumzo yoyote, yaliofikiwa." Msemaji huyo alisisitiza mbele ya waandishi wa habari.

Soma pia:Israel yaidhinisha operesheni ya kijeshi Rafah

Wizara ya Afya ya Gaza inayoongzwa na Hamas imesema kuwa mapigano katika eneo hilo yamesababisha vifo vya takriban Wapalestina 31,819, huku wanawake na watoto ni theluthi mbili ya wawalifariki.

Shirika la Umoja wa Mataifa lakuhudumia masuala ya chakula lilionya kwamba "njaa iko karibu" kuwakumba Wapalestina waliokimbia mashambulizi katika maeneo mengine ya Ukanda na kukimbilia kaskazini mwa Gaza.

Kwa habari nyingine, tafadhali tembelea chaneli yetu ya YouTube: