1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani haijaridhishwa na jawabu la Iran kuhusu nyuklia

2 Septemba 2022

Marekani haijaridhishwa na jawabu jipya la Iran kuhusiana na kuufufua mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, siku moja baada ya wapatanishi wa Umoja wa Ulaya kuwa na matumaini kwamba hatimaye watalifanikisha suala hilo.

https://p.dw.com/p/4GLrZ
USA Präsident Joe Biden in Philadelphia
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Hiki ndicho kizingiti cha hivi karibuni kati ya Marekani na Iran kupitia Umoja wa Ulaya, ambao mnamo mwezi uliopita wa Agosti ulifanikiwa kuuondoa mkwamo baada ya mazungumzo ya mwaka mmoja na nusu yaliyokuwa yanakwenda kwa kasi ya kobe.

Mnamo Agosti 8 Umoja wa Ulaya uliwasilisha kile ulichokiita waraka wa mwisho wa kuufufua mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015, ambao ulivunjwa na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Iran ilipendekeza mabadiliko kwa waraka huo, mabadiliko yaliyokubaliwa pakubwa na Umoja wa Ulaya na Marekani ikatoa jawabu lake kupitia kwa wapatanishi katika mazungumzo hayo.

Marekani haitaki IAEA kusitisha uchunguzi wake Iran

Na hapo Alhamis, Iran kupitia msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje Nasser Kanaani ilisema jawabu ililolituma kwa Marekani lilikuwa na lengo la kujenga hoja ya kukamilisha mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kuhusiana na mkataba huo.

Iran Atomanreicherungsanlage im Kernforschungszentrum Natanz
Kinu cha nyuklia IranPicha: AEO Iran/AFP

Ila Marekani ilitoa mtazamo tofauti. Imekataa kutoa taarifa zaidi hadharani kuhusiana na pingamizi lake ila miongoni mwa yale inayopinga ni msisitizo wa Iran kwamba Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA kusitisha uchunguzi wa maeneo matatu ambayo hayajawekwa wazi, yanayoshukiwa kuwa yanaendeleza shughuli za nyuklia, kabla kuafikiwa makubaliano ya kuufufua mkataba huo wa nyuklia wa mwaka 2015.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran hapo juzi alisema kwamba nchi hiyo inahitaji hakikisho kuu kutoka kwa Marekani kwa ajili ya kufufuliwa kwa mkataba huo na kuongeza kwamba uchunguzi wa IAEA wa shughuli za nyuklia za Iran umechochewa kisiasa.

Marekani ikirudi kwenye mkataba bei ya mafuta duniani itapungua

Katika mkataba huo wa mwaka 2015, Iran ilikuwa imesitisha mpango wake wa nyuklia kwa ajili ya kupunguziwa vikwazo na Marekani, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Österreich Wien | Internationale Atomenergie-Organisation | Rafael Mariano Grossi
Mkuu wa IAEA Rafael GrossiPicha: Lisa Leutner/AP Photo/picture alliance

Iwapo Rais Joe Biden atarudi katika mkataba huo, basi Marekani itaipunguzia Iran vikwazo kutokana na kukubali vikwazo vikali itakavyokuwa imewekewa na pia Marekani itasitisha juhudi za rais wa zamani Trump za kuyazuia mataifa mengine kununua mafuta ya Iran.

Hatua hii itaisababishia Iran kuweza kuuza zaidi ya mapipa milioni moja ya mafuta kwa siku, jambo litakalopunguza bei ya mafuta duniani iliyopanda baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Chanzo: AFP/Reuters