1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mar del Plata, Argentina. Waandamanaji wapambana na polisi wakipinga sera za Bush.

5 Novemba 2005
https://p.dw.com/p/CELr

Waandamanaji waliokuwa wakifanya ghasia wametia doa katika siku ya mwanzo ya mkutano wa mataifa 34 ya bara la Amerika jana Ijumaa wakati mataifa hayo yakigawika juu ya agenda inayohusu biashara huria inayopigiwa upatu na rais wa Marekani George W. Bush.

Polisi wa kuzuwia ghasia walifyatua mabomu ya gesi ya kutoa machozi wakati waandamanaji wakirusha mabomu ya petroli, wakiwasha moto barabarani , wakivunja madirisha ya maduka , kiasi cha mita 600 kutoka katika hoteli ambako viongozi walikuwa wakikutana katika mji wa kusini wa kitalii ulioko pwani.

Mamia ya waandamanaji wakijifunika nyuso zao walipambana na polisi baada ya kundi kubwa la watu wapatao 40,000 walipofanya maandamano yao kwa amani katika uwanja wa mpira ili kutoa malalamiko yao dhidi ya sera za rais Bush.

Polisi wa Argentina wamesema kuwa watu 64 wamekamatwa katika mapambano hayo katika mji huo wa Mar del Plata.

Migomo na maandamano dhidi ya Bush ilifanyika katika maeneo kadha nchini Argentina .