1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMali

Mapigano yazuka kati ya waasi wa Tuareg na jeshi la Mali

18 Septemba 2023

Mapigano mapya yamezuka kati ya jeshi la Mali na waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo kutoka jamii ya Tuareg, huku waasi hao wakidai kuchukua udhibiti wa kambi mbili za jeshi kwenye mji uitwao Lere.

https://p.dw.com/p/4WS5b
Wapiganaji wa kabila la Tuareg
Wapiganaji wa kabila la TuaregPicha: SOULEYMANE AG ANARA/AFP/Getty Images

Taarifa hizo kutoka upande waasi zilitolewa na msemaji wa muungano wa makundi ya waasi uitwao Coordination of Azawad Movements unaofahamika kwa harakati zake za kutaka kujitenga kwa eneo la kaskazini mwa Mali.

Jeshi la Mali nalo lilitoa taarifa kwamba shambulio limetokea kwenye mji wa Lere na liko njiani kwenda kujibu mapigo.

Muungano huo wa waasi wanaotaka kuunda dola ya Azawad kaskazini mwa Mali umekuwa ukipambana na jeshi tangu mwezi Agosti.

Mapigano yalichacha baada ya kuondoka kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ambao kwa miaka mingi walisaidia kuimarisha utulivu.

Mzozo kaskazini mwa Mali ulizuka mnamo mwaka 2012 na tangu wakati huo hujuma za waasi wa Tuareg zimesababisha ukosefu mkubwa wa usalama kwenye eneo hilo.