1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Juhudi za upatanishi zashika kasi ukanda wa Gaza

Sylvia Mwehozi
2 Februari 2024

Mapigano yameendelea Gaza na watu kadhaa wameuwawa usiku wa kuamkia leo siku moja baada ya Qatar kusema kwamba Hamas imetoa ishara ya awali ya makubaliano ya kubadilishana wafungwa na kusimamisha vita vyake na Israel.

https://p.dw.com/p/4bxQS
Wapalestina wakiishi katika kambi za muda kufuatia mapigano Gaza
Wapalestina wakiishi katika kambi za muda kufuatia mapigano GazaPicha: DW

Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, imesema, watu 105 wameuawa usiku wa kuamkia leo ijumaa.

Ofisi ya mawasiliano ya kundi hilo pia imeripoti uvamizi na mashambulizi ya makombora katika mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza.

Wakati huo huo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar, Majed al-Ansari alisema hapo jana kwamba mazungumzo ya hivi karibuni yaliyofanyika mjini Paris baina ya maafisa wa nchi hiyo, Marekani, Israel na Misri yamefanikisha pendekezo la pamoja la usuluhishi.

Mzozo wa kibinadamu pamoja na ongezeko la vifo vya raia, vimechochea kushamiri kwa miito ya kimataifa ya kusitisha mapigano.