1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Wizara ya Afya ya Gaza: Idadi ya Maafa yapita 27,000 Gaza

1 Februari 2024

Wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema idadi ya watu waliouawa katika Ukanda wa Gaza imepindukia 27,000 na kwamba 66,000 wamejeruhiwa kufuatia operesheni inayoendelea ya Israel katika ukanda huo.

https://p.dw.com/p/4bw1f
KUlingana na wizara ya Afya ya gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya vifo tangu uamuzi wa mahakama ya ICJ katika kesi iliyowasilishwa dhidi ya Israel, imeongezeka kwa zaidi ya watu 1000.
KUlingana na wizara ya Afya ya gaza inayodhibitiwa na Hamas, idadi ya vifo tangu uamuzi wa mahakama ya ICJ katika kesi iliyowasilishwa dhidi ya Israel, imeongezeka kwa zaidi ya watu 1000.Picha: Adel Al Hwajre/ZUMA Press/picture alliance

Wizara hiyo ya afya inayodhibitiwa na Hamas, imetoa takwimu hizo huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor akiishutumu Israel kwa kupuuza uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Haki ya Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, ulioitaka kufanya kila iwezalo kuepusha mauaji ya kimbari.

Idadi ya vifo imeongezeka kwa watu 1,100 tangu mahakama hiyo ya kimataifa iliyoko The Hague ilipotoa agizo hilo. Israel hukanusha tuhuma za mauaji ya kimbari zilizowasilishwa dhidi yake na Afrika Kusini kwenye mahakama hiyo.

Soma pia: Netanyahu: Sitaridhia makubaliano ya kusitisha mapigano

Kulingana na wizara ya afya ya Gaza, vifo hivyo vya hivi karibuni vimesogeza idadi ya vifo kufikia 27,019, bila kubainisha vifo vya raia na vya wanamgambo, lakini inasema baadhi ya waliouawa ni wanawake na watoto.

Jeshi la Israel lilisema vikosi vyake viliwaua wanamgambo 15 kaskazini mwa Gaza siku iliyopita na vililenga miundo mbinu ya wanamgambo hao shuleni.

Waziri wa mambo ya Nje wa Afrika Kusini aituhumu Israel kupuuza ushauri wa mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa mambo ya Nje wa Afrika Kusini aituhumu Israel kupuuza ushauri wa mahakama ya Haki ya Umoja wa Mataifa.Picha: REMKO DE WAAL/ANP/AFP/Getty Images

Mnamo Oktoba 7, Hamas, kundi ambalo Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya miongoni mwa nchi nyingine zimeliorodhesha kuwa la kigaidi, lilifanya shambulizi kusini mwa Israel na kuua watu 1,200, wengi wakiwa rai ana kuwashika mateka takriban 250. Hayo ni kulingana na mamlaka za Israel.

Hayo yakijiri Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na kundi la mabalozi katika Umoja wa Mataifa mjini Jerusalem. Amewaambia mabalozi hao ambao hususan ni wa nchi za Ulaya kwamba Hamas limejipenyeza katika shirika kuu la misaada kwa Wapalestina mjini Gaza na kwamba ni sharti shirika hilo lifungwe.

Soma pia: UN: Ni hatari kusitisha ufadhili kwa shirika la UNRWA

Matamshi ya Netanyahu yanafuata madai ya Israel kwamba wafanyakazi 12 wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa UNRWA walishiriki kwenye shambulizi la oktoba 7.

Majengo mengi yameharibiwa gaza kufuatia operesheni ya vikosi vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas.
Majengo mengi yameharibiwa gaza kufuatia operesheni ya vikosi vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas.Picha: Ahmad Hasaballah//Getty Images

Madai ambayo yalichochea nchi kadhaa kusitisha ufadhili wao kwa shirika hilo.

Katika tukio jingine linalofungamana na mzozo wa Mashariki ya Kati, mamlaka ya Uingereza ya baharini inayohusika na biashara (UKMTO) imesema mlipuko umeripotiwa karibu na meli, magharibi mwa Hodeidah nchini Yemen.

Hata hivyo mamlaka hiyo imesema meli hiyo pamoja na wahudumu wake wako salama.

Soma pia: Mzozo wa Gaza watishia kutanuka kote Mashariki ya Kati

Wakaazi walisema Wahouthi walifyatua makombora kutoka kambi iliyoko kwenye mji wa katikati ya Yemen Ibb, unaodhibitiwa na Wahouthi kuelekea Bahari ya Shamu.

Wahouthi wamekuwa wakifyatua wimbi la mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu kama jibu kwa operesheni ya Israel huko Gaza.
Wahouthi wamekuwa wakifyatua wimbi la mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu kama jibu kwa operesheni ya Israel huko Gaza.Picha: Indian Navy/AP/dpa/picture alliance

Katika wiki za hivi karibuni, wanamgambo wa Kihouthi walio na mafungamano na Iran, na wanaodhibiti maeneo yenye wakaazi wengi nchini Yemen, wamekuwa wakifyatua misururu ya droni na makombora dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu na katika Huba ya Aden, wakisema ni jibu operesheni ya Israel huko Gaza na pia kuonyesha mshikamano na Wapalestina.

Kampeni hiyo ya Wahouthi imevuruga safari za kimataifa za meli za kibiashara.

Marekani na Uingereza zimekuwa zikifyatua makombora kulenga miundo mbinu za Wahouthi nchini Yemen, na zimewarudisha wanamgambo hao katika orodha ya ‘makundi ya kigaidi'.

Vyanzo: APE, DPAE