1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea licha ya M23 kushindwa

4 Novemba 2013

Licha ya wito wa kusitisha mapigano uliotolewa na kundi la waasi la M23, wanajeshi wa Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameripotiwa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya maeneo waliko waasi hao.

https://p.dw.com/p/1AB7I
Wanajeshi wa Kongo wakiwa karibu na mji wa Goma mwanzoni mwa mwezi Septemba 2013.
Wanajeshi wa Kongo wakiwa karibu na mji wa Goma mwanzoni mwa mwezi Septemba 2013.Picha: Carl de Souza/AFP/Getty Images

Katika taarifa iliyotolewa na waasi hao na kunukuliwa na shirika la habari la AFP, M23 wamesema kwamba jeshi limeyashambulia maeneo ya milimani ambako kiasi cha wapiganaji 200 wamejificha tangu walipofurushwa kutoka ngome yao ya mwisho wiki iliyopita.

Hapo Jumapili (tarehe 3 Oktoba), kiongozi wa kundi hilo, Bertrand Bisimwa, alitaka kuwepo usitishaji wa mapigano, akiwaelekeza wapiganaji wake kuweka silaha zao chini na pia jeshi la Kongo kusitisha uhasama ili kuyaruhusu mazungumzo ya amani yaendelee.

Baada ya miezi 18 ya uasi ulioshuhudia waasi hao wakifanikiwa kwa haraka na kwa kipindi kifupi kushikilia mji wa Goma mwaka jana, jeshi la Kongo lilirudisha mashambulizi mwezi uliopita, na kuyarudisha haraka maeneo yaliyotwaliwa na waasi hao.

Kwa sasa Bisimwa anaripotiwa kuwapo nchini Uganda, ambako mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekuwa yakiendelea, ingawa kumekuwa na taarifa za kukwama mara kwa mara.

"Kimya cha Rwanda kimesaidia kushindwa kwa M23"

Wataalamu wa eneo la Maziwa Makuu wanasema kushindwa huku haraka kwa M23 kwenye uwanja wa vita na jeshi la Kongo linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kukiwa hakuna kauli yoyote kutokea Rwanda, kumelifanya kundi hilo kupapia roho yake.

Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.Picha: Reuters

"Kwa hakika, kukaa kimya kwa Rwanda wakati M23 wakishambuliwa na jeshi la serikali kumesaidia sana kwenye kushindwa kwao," alisema afisa mmoja wa ngazi za juu wa jeshi.

Kumekuwa na shinikizo kubwa sana kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda kutokea Marekani na Umoja wa Mataifa kwamba asichukuwe hatua yoyote wakati huu, chanzo hicho kimesema.

Hata hivyo, upinzani unaoneshwa na wapiganaji wachache waliobakia unaashiria kwamba matatizo ya Kongo bado kabisa hayajesha, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Kundi la M23 lilianzishwa na waasi wa zamani wa Kitusi ambao walikuwa wamejumuishwa kwenye jeshi la Kongo chini ya makubaliano ya mwaka 2009, lakini wakaasi Aprili mwaka 2012 wakidai kwamba mkataba huo haukuwa umetekelezwa kikamilifu.

Mara kadhaa Umoja wa Mataifa umekuwa ukiilaumu nchi jirani za Rwanda na Uganda kwa kuwasaidia waasi hao chini kwa chini, madai ambayo nchi zote mbili imeyakanusha.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf