1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAzerbaijan

Karibu wakimbizi 1,050 wakimbia Karabakh, waenda Armenia

25 Septemba 2023

Karibu wakimbizi 1,050 kutoka jimbo la Nagorno-Karabakh wamewasili nchini Armenia, baada ya operesheni ya kijeshi iliyofanywa na jeshi la Azerbaijan na hatimaye kuchukua udhibiti wa jimbo hilo linalozozaniwa.

https://p.dw.com/p/4WkyL
Kundi la kwanza la wakimbizi wapatao 30 waliokimbia Nagorno-Karabakh wakiwa katika hoteli moja wakikaguliwa kabla ya kuanza safari kwenda Armenia, Sept. 24, 2023.
Kundi la kwanza la wakimbizi wapatao 30 waliokimbia Nagorno-Karabakh wakiwa katika hoteli moja wakikaguliwa kabla ya kuanza safari kwenda Armenia, Sept. 24, 2023.Picha: Vasily Krestyaninov/AP Photos/picture alliance

Taarifa za kuondoka kwa wakimbizi hao zimetolewa na serikali ya Armenia, jana Jumapili.

Mashuhuda waliokuwa eneo la mpakani wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba idadi kubwa ya wakazi wa Nagorno-Karabakh walioweza kupata usafiri walikuwa wakiondoka kwenye jimbo hilo.

Watu wa jamii ya Armenia waliokuwa wakiishi kwenye jimbo hilo wanahofia kufukuzwa ama kisasi kutoka kwa utawala wa kibabe wa Azerbaijan kufuatia mzozo wa miongo kadhaa.

Armenia imesema pia kwamba magari 23 ya kubebea wagonjwa yaliwabeba wanajeshi wa Armenia waliojeruhiwa kutoka Nagorno-Karabakh kwenda nchini humo, yakisindikizwa na shirika la kimataifa la misaada la Msalaba Mwekundu.