1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya Hamas na Israel yaongezeka licha ya upatanishi

13 Mei 2021

Wapalestina walioonekana kuchoka wameadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa ramadhani wakati Hamas na Israel wakirushiana maroketi na makombora ya angani huku machafuko ya Wayahudi na Waarabu yakienea kote Israel.

https://p.dw.com/p/3tLkg
Palästina Israel Konflikt
Picha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Wanamgambo wa Kipalestina wamerusha maroketi zaidi katika mji wa Tel Aviv leo wakati ambapo Israel imeendeleza kampeni yake ya kurusha mabomu na pia kuandaa majeshi yake na magari ya kivita karibu na ukanda wa Gaza.

Mzozo huo ambao umeingia siku yake ya nne leo haujaonyesha dalili za kupungua na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kampeni hiyo ya kuishambulia Gaza itachukua muda.

"Mfumo wa ulinzi wa kuzuia mashambulizi unatuweka katika nafasi nzuri ya kushambulia na jeshi la Israel tayari limeshambulia mamia ya sehemu, hivi karibuni tutavuka malengo elfu moja. Tunaendelea kulishambulia kundi la Hamas na kuwalinda raia wetu wakati huo huo. Itachukua muda mwrefu ila kwa kuendeleza mashambulizi zaidi na kujilinda, tutalifikia lengo letu la kuleta utulivu katika taifa la Israel."

Kulingana na msemaji wa jeshi la Israel Jonathan Conricus, karibu maroketi 400 yaliyorushwa na Hamas kutoka Gaza hayakufika yalikolengwa kutokana na mfumo wa kuzuia mashambulizi wa Israel. Conricus anasema Israel imeshambulia karibu maeneo 600 katika Ukanda wa Gaza, ikiwemo maeneo ya kutengenezea roketi na hifadhi za silaha.

Israel I Luftverteidigungssystem Iron Dome fängt Raketen der Hamas ab
Maroketi yaliyorushwa na Hamas yakiwa yameingiliwa na mfumo wa Iron DomePicha: Mohammed Abed/AFP/Getty Images

Haya yote yanafanyika wakati ambapo Waislamu kote duniani wanaadhimisha sikukuu ya Iddi al Fitr ambayo kwa kawaida familia hujumuika na marafiki kusherehekea baada ya mwezi mzima wa kufunga chakula. Lakini huko Gaza, Ukanda ulio na jumla ya watu milioni mbili, furaha ya kawaida wakati wa sikukuu ya Iddi imegeuka na kuwa majonzi kwa baadhi huku madaktari wakisema kwamba wiki hii pekee watu 83 wameuwawa katika Ukanda huo.

Sherehe za Iddi hazikuwa za kawaida pia Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi pamoja na Israel kwenyewe ambako asilimia 21 ya Waarabu wachache ambao wana chimbuko la Palestina ila uraia wao ni wa Israel, wamejiunga na Waisraeli wengine kujificha kutokana na mashambulizi ya maroketi yanayorushwa na Hamas na wanamgambo wa kiislamu.

Machafuko hayo yamesababisha mashirika kadhaa ya ndege Ulaya kusitisha safari zake kuelekea Israel. Shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesimamisha safari zake kuelekea Tel Aviv hadi kesho na katika taarifa yake limesema linanuia kurudia safari hizo Jumamosi. Mashirika mengine yaliyositisha safari zake ni shirika la ndege la Uingereza British Airways, Virgin Atlantic na shirika la Uhispania Iberia. Mashirika ya ndege ya Marekani ndiyo yaliyoanza kusitisha safari hizo.