1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Mapigano makali yaripotiwa katika mji wa Bakhmut

13 Machi 2023

Mapigano makali yameripotiwa katika mji wa Bakhmut wakati pande zote katika vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine, zikijaribu kuudhibiti mji huo wa mashariki mwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Oao1
Ukraine Tschassiw Jar, bei Bachmut | Ukrainische Armee
Picha: Narciso Contreras/Anadolu Agency/picture alliance

Vikosi vya Ukraine vimekabiliwa na mashambulizi makali ya Urusi katika mji wa Bakhmut, ulioko katika mkoa wa mashariki wa Donetsk wakati pande zote katika vita hivyo zikidai kuwauawa wapiganaji wa pande pinzani.

Katika taarifa yao leo asubuhi, Jeshi la Ukraine limesema wapiganaji wa kundi la mamluki la Wagner wanajaribu kuvunja ngome za ulinzi za askari wa Ukraine na kuelekea katikati mwa mji.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa, wapiganaji wa Ukraine wamesababisha madhara na hasara kubwa kwa adui, ikimaanisha kundi hilo la mamluki wa Urusi ambao wanaongoza mashambulizi katika mji wa Bakhmut.

Soma pia:Ukraine yaamua kuendelea kuutetea mji wa Bakhmut 

Rais Volodymyr Zelenskiy amesema, "Katika muda wa chini ya wiki moja - tangu Machi 6 - katika eneo la Bakhmut pekee, askari wetu walifanikiwa kuwauwa maadui 1,100, ambapo ni hasara kubwa kwa Urusi.Kando na hayo, askari wengine 1,500 wa Urusi walijeruhiwa, na kuwaondoa katika uwanja wa mapambano. Pia vifaa vya kijeshi vya adui viliharibiwa."

Ama kwa upande wao, mkuu wa kundi la mamluki wa Wagner Yevgeny Prigozhin amesema kuwa, hali katika mji huo wa madini ni ngumu mno na kwamba kadiri wanavyozidi kukaribia katikati mwa mji, ndivyo mapambano yanavyozidi kuwa makali.

Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema jana kuwa, vikosi vyake vimewaua zaidi ya wapiganaji 220 wa Ukraine katika kipindi cha saa 24 katika mkoa wa Donetsk.

Rais wa China Xi Jinping kufanya ziara Moscow

China | Volkskongress (NPC) in Peking
Rais wa China Xi JinpingPicha: GREG BAKER/POOL/AFP/Getty Images

Wakati hayo yanaripotiwa, Rais wa China Xi Jinping anapanga kusafiri kuelekea Urusi ili kukutana na mwenzake Vladimir Putin, huku ziara hiyo ikitarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Shirika la Habari la Urusi la Tass, liliripoti mnamo Januari 30 kuwa Putin alimualika Xi mjini Moscow wakati wa majira ya machipuko. Mwezi uliopita, Jarida la The Wall Street la nchini Marekani liliripoti kuwa, ziara ya Xi mjini Moscow huenda ingefanyika aidha mwezi Aprili au mapema mwezi Mei.

Soma pia:Rishi Sunak na Emmanuel Macron kujadili uhamiaji na Ukraine 

Hata hivyo, Wizara ya mambo ya nje ya China haikujibu mara moja ombi la kuitaka kuthibitisha uwezekano wa Xi kufanya ziara ya Moscow. Kremlin pia haikuzungumzia ziara hiyo.

Hakuna maelezo mengine yaliyotolewa juu ya ziara hiyo. Vyanzo vilivyotoa taarifa hiyo vilikataa kutambulishwa kutokana na uzito wa suala hilo.

China na Urusi zilifikia makubaliano "yasiokuwa na kikomo" mnamo mwezi Februari mwaka jana, wiki chache tu kabla ya Urusi kuivamia Ukraine, na washirika hao wawili mara kwa mara, wametoa kauli za kuthibitisha uimara wa uhusiano wao.