1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano kati ya India na Pakistan yaendelea

Yusra Buwayhid
2 Machi 2019

Wanajeshi wa Pakistan na India kwa mara nyingine tena wameshambuliana katika vijiji vya eneo linalozozaniwa la Kashmir, na kusababisha vifo vya zaidi ya raia sita na wanajeshi wawili wa Pakistan.

https://p.dw.com/p/3EMWb
Indien Kaschmir Beisetzung CRPF Polizist in Srinagar
Picha: Reuters/D. Ismail

Wakati mvutano huo ukiwa umepamba moto kati ya mahasimu hao wawili wamiliki wa silaha za nyuklia, kauli ya waziri wa Pakistan ya kwamba huduma ya pamoja ya treni kati ya nchi hizo mbili itaanza tena kufanya kazi Jumatatu, imeashiria huenda hali hiyo ya mapigano ikatulia kidogo.

Waziri wa reli Pakistan, Sheikh Rashid Ahmed, amewaambia waandishi habari Jumamosi kwamba huduma ya haraka ya reli ya Samjhauta inayouunganisha mji wa Pakistan wa Lahore na mji wa mpakani wa Atari nchini India itaanza kufanya kazi tena kuanzia Jumatatu. Huduma hiyo ilisitishwa kufanya kazi na serikali ya Pakistan wiki iliyopita.

Mvutano umezidi kushika kasi tangu ndege ya India kuingia katika anga la Pakistan Jumanne iliyopita, iliyofanya kile kilichoelezwa na India kuwa ni shambulio la kustukizia dhidi ya wanamgambo wanaohusishwa na shambulio la mabomu la kujitoa muhanga la Febuari 14 katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India. Shambulio hilo limesababisha vifo vya wanajeshi 40 wa India.

Pakistan ililipiza kisasi, kwa kuidungua ndege ya kijeshi Jumatano na kumshikilia rubani wake, ambae baadae ,alikabidhiwa kwa serikali ya India Ijumaa kama ishara ya kutaka kutejesha amani.

Mapigano hata hivyo yalianza tena usiku kucha Ijumaa. Jeshi la Pakistan limesema wanajeshi wake wawili waliuawa katika makabiliano ya risasi za moto na vikosi vya India, karibu na mpaka unaozitenganisha pande mbili za Kashmir, unaosimamiwa na India na ule unaosimamiwa na Pakistan, huku kila upande ukidai umiliki kamili wa eneo hilo.

Wakati huo huo polisi nchini India, imesema ndugu wawili na mama yao waliuliwa katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India. Watu hao watatu waliuawa baada ya bomu lilovurumishwa na na wanajeshi wa Pakistan kupiga nyumba yao katika eneo la Poonch karibu na mpaka unaozitenganisha pande hizo mbili za Kashmir. Baba wa watoto hao pia alijeruhiwa vibaya.

Infografik Karte Kaschmirkonflikt PT
Ramani ya eneo la mzozo katika Kashmir iliyogawanyika

Na katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na Pakistan, afisa wa serikali Umar Azam amesema wanajeshi wa India waliojihami kwa silaha nzito wamekuwa wakivilenga vijiji vya upande wao karibu na mpaka huo bila ya kubagua na kusababisha kifo cha mtoto mmoja wa kiume na kuwajeruhi watu wengine watatu. Ameongeza kwamba nyumba kadhaa pia zimeharibiwa na mashambulizi hayo ya mabomu yaliyofanywa na wanajeshi wa India.

Kufuatia masaa machache ya utulivu, mashambulizi ya mabomu na ya kutumia silaha ndogo ndogo yalianza tena Jumamosi. Taarifa ya jeshi la Pakistan imesema raia wao wawili waliuawa na wengine wawili walijeruhiwa katika mapigano hayo. Jeshi la India lilisema wanajeshi wa Pakistan walivishambulio vituo vyao kadhaa katika eneo hilo linazozitenganisha pande mbili za Kashmir.

Urusi yataka kuwa mpatanishi

Tokea mapigano kupamba moto kufuatia shambulio la kujitoa muhanga la mwezi uliopita, viongozi wa mataifa mbalimbali wamekuwa wakijaribu kutuliza hali ili kusije kukazuka vita kati ya India na Pakistan. Tokea kupata uhuru wao kutoka Uingereza 1947, vita viwili kati ya vitatu walivyopigana mahasimu hao vilikuwa ni kuhusu eneo la Kashmir.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema Jumamosi kwamba Urusi imejitolea kuwa mpatanishi wa mzozo huo. Amesema Pakistan iko tayari na imelikubali pendekezo hilo la Urusi, lakini hana uhakika iwapo India nayo itakubali kwa upande wake.

Qureshi pia amesema mwanadiplomasia wa Saudi Arabia atazitembelea India an Pakistan. Maafisa wa Pakistan wamesema China inatarajiwa kutuma ujumbe India na Pakistan wiki ijayo.

Vurugu zinazoendelea hivi sasa ni mbaya zaidi kushuhudiwa katika mvutano ulionza kufukuta chini kwa chini tangu 1999, pale jeshi la Pakistan lilipotuma kikosi cha ardhini katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India. Mwaka huo huo pia ndege ya kijeshi ya India iliidungua ndege ya jeshi la anga la Pakistan na kupelekea watu wote 16 waliokuwamo ndani yake kuuawa.

Wimbi la hivi karibuni la mapigano limeanza baada ya kundi la wanamgambo Jaish-e-Mohammad kudai kuhusika na shambulio la mabomu la kujitoa muhanga la Febuari 14 katika ardhi ya Kashmir inayodhibitiwa na India. India kwa muda mrefu imekuwa ikiishutumu Pakistan kwa kuunga mkono makundi ya kigaidi kufanya mashambulizi dhidi yake. Pakistan hata hivyo, imekana kuhusika kwa namna yoyote ile katika shambulio hilo la kujitoa muhanga.

Maelfu ya watu wa pande zote mbili za Kashmir wameyahama makaazi yao na kukimbilia katika makaazi ya muda yanayosimamiswa na serikali, na wengine wamekimbilia kwa jamaa zao wanaoishi katika maeneo yaliyo salama zaidi wakikimbia eneo linazozitenganisha pande hizo mbili ambalo limegawanywa kwa uzio wa senyenge na minara ya uangalizi. Eneo hilo liko katikati ya misitu pamoja na mashamba ya mpunga na mahindi.

(AP,dpa)