1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapadre 25 wamefariki Tanzania katika miezi 2

3 Machi 2021

Kanisa Katoliki nchini Tanzania limesema mapadre wake wapatao 26 wamefariki dunia katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na matatizo ya upumuaji

https://p.dw.com/p/3q8S7
Kenia katholische Kirche in Garissa
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Hali hii imelifanya kanisa hilo kulazimika kutoa mwongozo mpya kwa waumini wake wakati huu wa kuelekea maadhimisho ya Pasaka.

Kanisa hilo lenye idadi kubwa ya waumini nchini, limesema mbali ya kupoteza makasisi wake hao, pia watawa wake yaani masista na waauguzi wapatao 60 nao wamefariki dunia katika kipindi hicho hicho na wote wanatajwa kukumbwa na tatizo la aina moja linalohusiana na mifumo ya upumuaji.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu nchini, Padre Charles Kitima ambaye amekutana na waandishi wa habari leo, hali kama hiyo siyo ya kuwaidi kuwahi kushuhudiwa na kanisa hilo hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inaendelea kukabiliwa na wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya corona.

Kanisa linaendelea kuzingatia mwongozo wa wizara ya afya

Kanisa hilo limesema linatambua dunia inapitia katika wakati mgumu na hakuna muujiza mwingine unaoweza kuinusuru mbali ya kuendelea kumwomba Mungu lakini wakati huo huo kuendelea kuzingatia maagizo ya kisayansi na wataalamu wa afya.

Limesema linaendelea kuzingatia miongozi inayotolewa na wizara ya afya kuhusu kujikinga na maambukizi hayo, lakini limelazimika kwenda mbali zaidi kuwahimiza waumini wake kutambua kuwa janga hilo lipo.

Kuhusu maadhimisho ya kuelekea Sikukuu ya Pasaka, Kanisa hilo limetoa mwongozo mpya unaowataka waumini wake kutumia nyenzo zote zitakazowaweka mbali na maambukizi ya virusi vya corona.

Maoni ya Watanzania juu ya Covid 19 na chanjo yake

Mbali na hilo, kanisa hilo limewatolea mwito watafiti wa tiba na wanasayansi nchini kujitokeza kusaka chanzo cha kuwepo kwa ongezeko la visa vinavyohusiana na matatizo ya upumuaji.

Kuendelea kufanya mzaha ni hatari sana

Wakati hayo yakiwa hivyo, nalo Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limesitisha mara moja matamasha yote yanayoambatana na maadhimisho ya Pasaka kama hatua mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid 19.

Kanisa hilo limeonya kuwa, kuendelea kufanya mzaha katika janga kama hilo ni hatari na kusisitiza kuwa elimu ya kutosha inapaswa kuendelea kutolewa kwa kila mwananchi.

Makanisa hayo mawili ndiyo yaliyokuwa ya kwanza kabisa tangu kuzuka kwa wimbi jipya la maambukizi ya virusi vya Corona kutoa waraka ukiwaonya waumini wake kuchukua tahadhari juu ya janga hilo.

Katika hatua nyingine, kumekuwa na hoja zinazoanza kuibuka kuhusu hatma ya waumini wa dini ya Kiislamu wanaokusudia kwenda kuhiji Makkha, hasa baada ya mamlaka nchini humo kuonya kuwa hakuna muumini atayeruhusiwa kuingia nchini humo kwa ajili ya Hija kama atakuwa hajapata chanjo ya virusi vya corona.