1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Wahafidhina wa CDU njia panda

16 Machi 2021

Baada ya matokeo mabaya ya kihistoria katika chaguzi za majimbo za Baden-Württemberg na Rhineland Palatinate, Wahafidhina Ujerumani wanastahili kujitazama upya, anaandika Marcel Fürstenau.

https://p.dw.com/p/3qgd0
Weltspiegel 05.03.2021 | Corona | Deutschland Berlin | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Haijawahi kutokea kabisa chama cha Christian Democratic Union CDU kupata matokeo mabaya kiasi hiki katika uchaguzi kwenye majimbo ya Baden-Württemberg na Rhineland Palatinate. Siku za kwamba majimbo yote hayo ni ngome za Wahafidhina na kwamba chama cha CDU kitashinda kwa wingi, zimepita.

Kwa sasa chama hicho kimepata chini ya asilimia 30 ya kura katika kitakachowapelekea wanachama wengi wa chama hicho waingie hofu kwamba ndivyo itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba.

Wabunge waliziweka tamaa zao mbele ya chama

Huku ikiwa nusu mwaka tu ndio uliosalia, chama hicho kinastahili kujiuliza kitairudisha vipi imani ya wapiga kura huku kura za maoni kote Ujerumani zikionyesha kuwa chama hicho kinapoteza uungwaji mkono. Deutschlandtrend ambao ni mtandao unaoonyesha maoni ya kisiasa kwa kila chama Ujerumani kila mwezi, unakiweka chama cha CDU na chama chake ndugu cha Christian Social Union CSU vikiwa na asilimia 33 tu.

Na ufichuzi wa hivi majuzi kwamba wabunge wa vyama hivyo waliziweka tamaa zao mbele kwa kujinufaisha binafsi kifedha kutokana na uuzaji wa barakoa, ni mambo ambayo kwa kweli yatazidi kuchangia huku kushuka uungwaji mkono.

Deutschland CDU Gremiensitzungen und Statements der Bundesparteien
Kiongozi wa chama cha CDU Armin LaschetPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Chama cha wanamazingira cha Kijani huko Baden-Württemberg lakini kina mambo mengi yanayowiana na chama cha CDU, ambapo wanakubaliana katika misimamo yao mingi ya kihafidhina. Chama hicho cha Kijani kina hamu sana ya kuwa sehemu ya serikali ya shirikisho baada ya uchaguzi mkuu wa Septemba.

Wadadisi wanataka kujua atakayechukua mikoba kutoka kwa Angela Merkel

Na hicho ni kitu ambacho wanaweza kukipata tu na vyama vya CDU na CSU kwasababu licha ya uungwaji mkono wa vyama hivyo kushuka, inaonekana hakuna njia nyengine ya serikali ya Wahafidhina na Wanamazingira baada ya Angela Merkel kuondoka madarakani.

Licha ya yote haya, wadadisi ndani ya  Ujerumani na Kimataifa wanataka kujua ni nani atakayefuata nyayo za Angela Merkel iwapo Wahafidhina wataongoza serikali baada ya uchaguzi wa Septemba, licha ya kupoteza kunakotarajiwa. Kiongozi wa CDU Armin Laschet na waziri mkuu wa Jimbo la Bavaria Markus Söder wa CSU ndio wanaopigiwa upatu.

Mmoja wao atachaguliwa kama mgombea. Wahafidhina wakichagua mgombea wao mapema basi kuna nafasi yao kuwapelekea wapiga kura wasahau sakata zilizopita kwa haraka. Na Wanamazingira nao watajua wanachotarajia iwapo matokeo yatawakubalia kuunda muungano.