1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mwendokasi wa hatifungani za Korona

19 Mei 2020

Ujerumani na Ufaransa zinataka kuuongoza Umoja wa Ulaya kutoka kwenye mzozo uliosababishwa na janga la virusi vya korona kwa kuwa na mfuko wa pamoja wa madeni, lakini Bernd Riegert anasema huu ni mchezo wa bahati nasibu.

https://p.dw.com/p/3cSZ5
Berlon | Videokonferenz Emmanuel Macron und Angela Merkel
Picha: Reuters/K. Nietfeld

Hatimaye, treni ya Ujerumani na Ufaransa kwenye Umoja wa Ulaya ilikuwa imeanza tena kutembea kwa mwendo wa kasi. Lakini Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wameweka gia ya kurudi nyuma ili kwanza kuutatuwa mzozo uliosababishwa na janga la virusi vya korona kwenye Umoja huo. Kansela sasa amebadilisha mwelekeo ambapo kimsingi anakubaliana na mfuko wa pamoja wa madeni, licha ya marufuku ya madeni kwenye mikataba inayouunga Umoja wenyewe.

Rais wa Ufaransa amehakikisha kwamba kitita cha euro bilioni 500 cha ujenzi mpya baada ya korona kinatolewa kama msaada na wala sio mkopo kwa mataifa ya kusini mwa Ulaya ambayo tangu hapo tayari yameelemewa na madeni, kama anavyotaka Kansela Merkel na mataifa ya Nordic ndani ya Umoja wa Ulaya. Kwenye hili, Macron alipaswa kutambuwa kwamba mfuko wa maendeleo hauwezi kufikia kiwango cha euro trilioni 1.5 zilizotakiwa, bali ni robo yake tu.

Bernd Riegert, Korrespondent, Studio Brüssel
Bernd Riegert, DW Brussels

Ushirikiano wa Ujerumani na Ufaransa, kwa hivyo, umetowa pendekezo moja tu, ambalo nalo, hata hivyo, lilishakubaliwa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, ambayo sasa inayashinikiza mataifa mengine wanachama kutoka mashariki na kaskazini kuutekeleza.

Mataifa hayo, lakini, yatapata fedha haba kutoka mfuko wa ujenzi mpya baada ya korona, ila yatapaswa kulipa zaidi, hasa kwa nchi kama Italia, Uhispania na Ufaransa yenyewe, ambazo zimeathirika vibaya zaidi kwa korona.

Mshikamano zaidi

Mshikamano sasa utaombwa na mataifa kama Poland, Hungary, Bulgaria na Romania, ambayo daiam yamekuwa wapokeaji fedha kutoka Umoja wa Ulaya. Ndiyo maana Kansela Merkel alikubaliana na mataifa wanachama kutoka Mashariki kuifafanuwa nadharia yake.

Hapa nyumbani, Kansela Merkel atalazimika kupambana kikwelikweli, maana kwenye vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU lazima kutakuwa na upinzani mkali dhidi ya dhana ya kutowa ruzuku, kwani inamaanisha matumizi makubwa zaidi juu ya kiwango cha kawaida. Fedha zinapaswa kutolewa kupitia madeni ya pamoja, na Kamisheni ya Ulaya ndiyo inayokopa.

Mataifa wanachama yanalazimika kulilipa deni lote pamoja ndani ya kipindi cha miaka 20, kwa mujibu wa mgawo wao kwenye bajeti ya Umoja wa Ulaya. Kwa hivyo, uamuzi unaofanywa leo utaendelea kuzitanza serikali na mabunge hadi mwaka 2040 na kuzilazimisha kuweka ukomo wa bajeti zao.

Dhana hii mpya inaweza kuitwa kama hatifungani za Umoja wa Ulaya au hatifungani za korona. Hizi ni hatifungani zenye kiwango maalum cha mkopo. Lakini dhana hii inaweza kukiuka Kipengele 311 cha Mkataba wa Umoja huo.

Kuna ujanjaujanja mwingi ndani yake ambao unahitaji wanasheria kuweza kuuweka sawa. Kwa sasa Ufaransa na Italia zinaweza kushangiria kwamba zimeshinda. 

Lakini je, hii ni dhana itakayofanya kazi kweli? Kwa Kansela Merkel na Rais Macron jibu ni ndiyo, kwa sababu kwenye hali kama hii ya kipekee, unapaswa kuchukuwa hatua na sio kusitasita.

Kwa hivyo, sasa treni ya Ujerumani na Ufaransa imeshika njia sahihi. Lakini suala ni je mabehewa yote, wanachama wote wa Umoja wa Ulaya, nayo yamefungashwa vyema?