1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Msaada wa NATO na Magharibi kwa Ukraine hautoshi

7 Machi 2022

Mataifa ya Magharibi yanajaribu kila uchao kuonesha mshikamano wao na Ukraine, lakini msaada huo hautoshi na hatima ya taifa hilo linalopambana na uvamizi wa Urusi inaonekana kuwa mashakani, anasema Barbara Wesel.

https://p.dw.com/p/486Q2
Brüssel | Sondertreffen NATO-Außenminister
Picha: Olivier Douliery/AFP/Getty Images

Ikiwa kauli za mshikamano zingeliweza kugeuka vifaru, mizinga ya kutungulia ndege ama ndege za kijeshi, yumkini hali ya Ukraine ingelikuwa na afadhali kidogo. Lakini tunachoona ni wingi wa maneno na uhaba wa msaada wa kijeshi. Na wanasiasa wetu wanatutayarisha kwamba fadhaa ya Ukraine ndio kwanza ipo mwanzoni. 

Baada ya mazungumzo yake ya karibuni kabisa kwa njia ya simu na Vladimir Putin, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema takribani vile vile alivyosema Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, siku ya Ijumaa mjini Brussels, kwamba hali itakuwa mbaya zaidi. 

Videostill | G20 | Barbara Wesel berichtet aus Rom
Barbara WeselPicha: DW

Taarifa za kijeshi zinakisia kwamba jeshi la Urusi karibuni litazidisha mashambulizi yake dhidi ya raia. Wenye mashaka wanakhofia kwamba mbabe huyo wa kivita ataufyeka mji mkuu, Kyiv, augeuze kifusi kama alivyoifanya Grozny. Kwa amri ya Putin, mji mkuu huo wa Chechenya uligeuzwa jalala tu mwaka 1999.

Kilio cha msaada kwa NATO

Akiwa anakabiliwa na wasiwasi huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekuwa akitaka iwekwe marufuku ya ndege kuruka kwenye anga la Ukraine, na Jumuiya ya Kujihami ya NATO imeshamjibu si mara moja wala mbili kwamba haiwezi kufanya hivyo, maana hilo litamaanisha kukabiliana moja kwa moja kijeshi na Urusi na, hivyo, kuchochea Vita vya Tatu vya Dunia. 

Tayari Putin ameshatukumbusha kuhusiana na silaha zake za nyuklia na amegusia kwamba huenda akaenda mbali zaidi kuifanya ndoto yake ya Himaya Kubwa ya Urusi, ikiwemo Ukraine, kuwa kweli. Wendawazimu wa mkuu huyu wa Kremlin ni jambo jengine la kutufanya tuwe tafrani.

Wengine wanamini kwamba NATO inapaswa kuwa na hadhari zaidi ili kuepusha vita vya kinyuklia. Hata kuwafikishia silaha Ukraine kunaweza kutafsiriwa na Putin kama ni kuchupa mpaka. Marekani, kwa upande mwengine, inaamini kwamba lazima Putin azuiwe sasa ili asije akafunuwa sanduku la machafuko na vita, kama alivyosema waziri wake wa mambo ya kigeni, Anthony Blinken. Kama ilivyo wa wengine, naye pia anakisia kuwa Putin anataka kuzishambulia nchi nyengine: Georgia, Moldova na mataifa ya Baltiki.

Mataifa ya Magharibi yamejibu hatua hii ya Putin kwa kumuwekea vikwazo vikali kabisa vya kiuchumi katika historia yake. Lakini ikiwa kweli tunataka kulizuwia treni la mauaji la Putin, tunapaswa kukaza nati zaidi.

Umoja wa Ulaya umetangaza sasa kwamba utazifungia benki, meli na bidhaa nyengine zaidi kuanzia wiki ijayo. 

Baada ya hapo, hatua ya mwisho itakuwa ni kuzuwia mafuta, gesi na makaa ya mawe kutoka Urusi. Lakini hilo litasababisha chumi zetu kudidimia zaidi na kuhatarisha usalama wa nchi zetu.

Ila kwenye hali ya mashaka kama hii, tutapaswa kukabiliana nayo, kwa sababu njia nyengine zozote ni mbaya zaidi.