1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan na mwisho mchungu wa "Amerika kwanza"

2 Machi 2021

Mwaka mmoja uliopita, Marekani ilifikia makubaliano na kundi Taliban, lakini hayakuhusu Afghanistan, bali njozi ya Donald Trump ya "Marekani Kwanza", na matokeo yake yamekuwa ni balaa tupu, anaandika Sandra Petersmann.

https://p.dw.com/p/3q5Ry
Afghanistan Zabul - U.S. Soldat
Picha: picture-alliance/dpa/ISAF

Bahati mbaya sana juu ya meza pana mambo mawili tu ya kuchaguwa: kuondosha wanajeshi wote wa kigeni kufikia tarehe 1 Mei kama ilivyokubaliwa kwenye Makubaliano ya Doha, au kuongeza muda wa uvamizi wa majeshi hayo ulioongozwa na Marekani ulioanza miaka 20 iliyopita. Binafsi napendelea wabakie, na wacha nikupe sababu zangu.

Majeshi ya kimataifa hayatashinda vita hivi, wala hayataweza kuleta amani. Lakini wanasalia kuwa nyenzo ya kusaka makubaliano kwenye mazungumzo magumu ya kusaka amani kwenye mji mkuu wa Qatar.

Soma pia: Ripoti: Mashambulizi ya Taliban yanaongezeka

Kwa hamu yao ya kutaka madaraka na kutambuliwa, Taliban wanataka ukaliwaji unaosimamiwa na majeshi ya kigeni ukome na kulegezwa kwa vikwazo dhidi yao. Haya ndiyo mambo mawili pekee ambayo mataifa ya Magharibi wana nguvu nayo katika kuwashinikiza wapiganaji hao wa siasa kali kusitisha mapigano na kuendelea na mazungumzo.

DW Kommentatorenbild Sandra Petersmann
Mwandishi wa DW Sandra Petersmann.Picha: DW/R. Oberhammer

Kwa ufasaha zaidi, kuondoka wanajeshi na vikwazo si dawa inayoweza kutibu kwa usiku mmoja. Watu wataendelea kufa nchini Afghanistan katika miezi ijayo kwa sababu ya ugaidi na vita. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, baina ya mwezi wa Oktoba na Disemba mwaka jana, raia 30 walikuwa wakiuawa ama kujeruhiwa kila siku.

Huu ni ukweli mchungu juu ya sera ya "Marekani Kwanza." Rais wa zamani, Donald Trump, aliichukuwa sera hiyo hadi kwenye ukomo wake kwa Makubaliano hayo ya Doha. Alitaka kujitwika sifa ya kuwa rais pekee kwenye historia ya Marekani kuweza kuwarejesha wanajeshi nyumbani. Alitaka kukomesha vita vya muda mrefu vya Marekani ili ashinde uchaguzi tu. Lakini hilo likamuojea.

Soma pia: Mazungumzo ya amani ya Afghanistan yawa ana kwa ana

Trump hakuwa wa kwanza kuamua juu ya majaaliwa ya Afghanistan kwa kutegemea pekee siasa za ndani. Hilo la "Marekani Kwanza" lilianza na uvamizi uliotokana na hisia za kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11.

Ndiyo, kwani ni kwa jinsi gani nyengine tunaweza kuelezea ushirikiano usio maadili kati ya Marekani na washirika wake wa Kimagharibi na wahalifu wa kivita na wavunjaji wa haki za binaadamu, kama vile Abdul Rashid Dostum, kwa sababu tu ya kuwawindaAl-Qaida na kuwaadhibu Taliban?

Uvamizi huo wa kukurupuka haukuzingatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 1978 nchini Afghanistan na ambavyo hadi leo havijatatuliwa. Wala uvamizi huo haukuzingatia angalau yale majeraha yaliyoachwa na Vita Baridi na ukaliaji kimavabu wa Wasovieti.

Kampeni ya kijeshi ilifanyika bila kuwazia dhima ya hatari waliyonayo majirani wa Afghanistan kwa taifa hilo, kama vile Iran, Pakistan  na India, ambao nao pia wanachochea mapigano kwa kiburi chao cha hali ya juu cha utaifa.

Ndio maana, licha ya kutimia sasa miaka 20 ya vita vya washirika wa Marekani na baada ya miongo minne ya vita dhidi ya watu wa Afghanistan, bado hakuna mambo yaliyo bora zaidi kuchaguwa kwenye meza ya mazungumzo.

Soma pia:Serikali ya Afghanistan na Taliban wazungumza Doha

Washirika wa Marekani, ikiwemo Ujerumani, watafuata mapigo ya mrithi wa Trump, utawala wa Joe Biden. Ikiwa Marekani itaondoka, vikosi vya washirika navyo vitaondoka. Kwa sasa, kuna wanajeshi 10,000 waliosalia nchini Afghanistan. Ikiwa Wamarekani watabakia, washirika wa NATO pia watabakia, ambapo  Ujerumani ina wanajeshi 1,100, ikiwa ya pili kwa kuwa na wajeshi wengi baada ya Marekani.

Lakini kutuma wanajeshi Afghanistan hakukupendwa Ujerumani kama kulivyochukiwa Marekani. Wajerumani pia wanauliza kwa nini jeshi lao bado liko huko, na wakati uchaguzi mkuu ukikaribia, wanasiasa mjini Berlin hawataki kuharibu kampeni zao kwa suala la Afghanistan - na wanakataa kutoa ufafanuzi unaohitajika. Nao pia wanaamini kwenye Ujerumani Kwanza!