1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Je Ujerumani itabadili msimamo wake dhidi ya Urusi?

3 Septemba 2020

Kansela Merkel ametaka majibu kamili juu ya "jaribio la mauaji" kwa kumpa sumu kiongozi wa upinzani wa Urusi, Alexei Navalny, ikimaanisha msimamo wa Ujerumani kuelekea Urusi umekuwa mkali, kama anavyoandika Jens Thurau.

https://p.dw.com/p/3hx8n
Deutschland Merkel PK Navalny
Picha: Getty Images/AFP/M. Schreiber

Tangu kiongozi huyo wa upinzani wa Urusi kuwasili kwenye Hospitali ya Cherite kwa ajili ya matibabu ikishukiwa kuwa amelishwa sumu, kumekuwa na uvumi mwingi juu ya hatua ambayo serikali ya Ujerumani ingelichukuwa. Mengi yalisemwa juu ya uwezekano wa kuonesha hasira za waziwazi, lakini si Kansela Merkel wala waziri wake wa masuala ya kigeni, Heiko Maas, aliyeonekana tayari kuichukulia hatua Urusi. Sasa hilo limebadilika.

Kwanza, serikali ya Ujerumani ilitowa kauli ya wazi na isiyo utata ikisema vipimo vya maabara vimegunduwa kwamba Navalny "bila shaka yoyote" alikuwa amepewa sumu ya jamii ya Novichok, ambayo huuwa mishipa ya fahamu.

Russland Moskau Nawalny
Kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexai NavalnyPicha: Reuters/T. Makeyeva

Kisha, Waziri wa Mambo ya Nje, Heiko Maas, na mwenzake wa ulinzi, Annegret Kramp-Karrenbauer, walijitokeza mbele ya waandishi wa habari kusema kwamba balozi wa Urusi alikuwa ameitwa "kujadiliana naye masuala muhimu.”

Mwisho, Kansela Merkel mwenyewe alijitokeza mbele ya waandishi wa habari kuelezea kutoridhishwa kwake, akisema kupewa sumu kwa Navalny lilikuwa "jaribio la mauaji."

Serikali imeweza kuweka wazi kwamba jaribio hilo lilikuwa pigo la karibuni kabisa kwenye msururu wa matukio yanayofanywa na Urusi – kuanzia kuichukuwa Rasi ya Crimea hadi kuwatia nguvuni na kuwauwa wapinzani wa kisiasa wa Urusi wakiwa katika ardhi ya Ujerumani, na hadi kampeni za upotoshaji zinazowalenga wapigakura nchini Ujerumani na hata kwenye eneo zima la Umoja wa Ulaya.

Madaktari wa Hospitali ya Charite walitoa taarifa wakisema kwamba Navalny bado ana hali mbaya kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, ambako anapumulia mashine na huku kupona kwake kukitarajiwa kuchukuwa muda mrefu sana kwa jinsi ya hatua aliyokuwa amefikia. Hapana shaka, huwezi kuwazia kitu kibaya zaidi ya sumu inayoshambulia mishipa ya fahamu.

Kommentatorenfoto Jens Thurau
Mwandishi wa DW Jens ThurauPicha: DW

Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya zitapaswa sasa kuchukuwa hatua za wazi dhidi ya Urusi. Moscow lazima iwataje kwa majina wahusika na hatimaye ichunguze jaribio hili la mauaji dhidi ya Navalny. Isipofanya hayo, basi vikwazo vipya lazima viwekwe.

Kwa hilo, ni wazi serikali mjini Berlin itakuwa inajaribu jambo gumu. Maana kamwe hatujuwi kipi ambapo Rais Vladimir Putin wa Urusi atakifanya pale atakapojikuta akiandamwa kwa shinikizo kali, ama iwe ni Belarus au Syria ama popote ambapo Moscow inajaribu kutanuwa misuli yake.

Hata hivyo, jibu hili kali kwa Urusi ni la muhimu sana ikiwa maafisa wa Ujerumani na Umoja wa Ulaya wanataka kubakia wakweli kwenye maadili ya uhuru wanayoyahubiri.

Wiki chache zijazo zitatupa jawabu.

Mwandishi: Jens Thurau