1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manusura wa Shakahola wafutiwe mashitaka- KNHCR

16 Juni 2023

Tume ya kitaifa nchini Kenya ya kutetea haki za kibinaadamu - KNHCR imeitaka serikali kufuta mashtaka yoyote dhidi ya manusura 65 wa mkasa wa shakahola waliofikishwa mahakamani jana.

https://p.dw.com/p/4Sft4
Wafanyakazi wakipokea miili iliyofukuliwa kwenye msitu wa Shakahola, inayoaminiwa kuwa ya waumini wa kanisa la  "Good News International Church"
Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Tume hiyo imeeleza kuwa badala ya kuwakamata, manusura hao wanapaswa kupewa ushauri nasaha na msaada wowote wanaohitaji kwa sasa pamoja na kujumuishwa katika jamii. Wahanga 64 waliahidi mahakama ya Shanzu, mjini Mombasa Kenya kuwa watazingatia usaidizi wanaopewa ikiwemo kuanza kula huku mmoja kati yao akikataa.

Soma Zaidi: Waliokufa kwa kuacha kula Kenya wapindukia watu 300

Waliruhusiwa kurudi kwenye kituo cha uokoaji cha Sajahanadi Mtwapa na mmoja aliyekataa kushirikiana na maafisa akapelekwa rumande. Hakimu Mkuu mwandamizi wa mahakama ya Shanzu Joe Omido alitoa amri kuwa kila mwathiriwa afanyiwe uchunguzi wa kiakili na ripoti za matibabu ziwasilishwe mahakamani baada ya siku 14. Manusura hao walifikishwa mahakani baada ya kugoma kula na kunywa kwa siku kadhaa wakiwa wanahifadhiwa katika kituo cha uokoaji. Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani kati ya tarehe 20 Juni na tarehe 29 Juni mwaka huu.