1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Neuer kurejea dimbani baada ya kukaa nje kwa mwaka mzima

27 Oktoba 2023

Nahodha huyo wa Ujerumani na Bayern Munich hajacheza tangu alipopata jeraha la mchezo wa kuteleza kwenye theluji Disemba mwaka jana baada ya kombe la dunia

https://p.dw.com/p/4Y7qA
Manuel Neuer anatarajiwa kurejea dimbani kesho katika mchezodhidi ya Darstadt
Manuel Neuer anatarajiwa kurejea dimbani kesho katika mchezodhidi ya DarstadtPicha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Nahodha na mlinda mlango wa Bayern Munich, Manuel Neuer atarejea katika mechi ya Jumamosi ya Bundesliga dhidi ya Darmstadt, baada ya kukosa takribani mwaka mmoja kutokana na kuvunjika mguu, kocha Thomas Tuchel amesema leo katika mkutano na waandishi wa habari.

Soma zaidi:Kipa Manuel Neuer asubiri kwa hamu kurudi dimbani

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37, kapteni wa Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani mwaka 2014, hajacheza tangu alipopata jeraha la mchezo wa kuteleza kwenye theluji Disemba mwaka jana, siku chache baada ya kurejea kutoka kuichezea nchi yake kwenye Kombe la Dunia nchini Qatar.

Kocha wa Bayern Munich Thomas Tuchel
Kocha wa Bayern Munich Thomas TuchelPicha: Martin Sylvest/AP Photo/picture alliance

"Mradi hakuna kitakachotokea katika mazoezi, atacheza kesho," Tuchel aliwaambia wanahabari katika mkutano na wanahabari. 

"Amefurahia, tumefurahi, na wengine watafurahi pia," Tuchel alisema huku akitabasamu.

Neuer hajaichezea Bayern tangu ushindi ugenini dhidi ya klabu yake ya zamani Schalke mnamo Novemba 12 mwaka jana, kabla ya Kombe la Dunia.

Soma zaidi:Kane: Bayern itazidi kuimarika msimu unavyosonga

Baada ya kuumia,alifanyiwa upasuaji mwezi Disemba na Bayern walimsajili mlinda mlango wa Uswizi Yann Sommer kutoka Borussia Moenchengladbach kuchukua nafasi ya Neuer, lakini aliondoka kwenda Inter Milan mwishoni mwa msimu.

Wachezaji wenzake wanamsubiri kwa hamu na bashasha

Beki Matthijs de Ligt alisema siku ya Jumatatu kuwa timu yao inasubiri kwa hamu kurejea kwa Neuer. Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Bayern walikuwa "na furaha sana kwamba Manu atarejea hivi karibuni" huku akimtaja kama "kipa wa kiwango cha dunia, mmojawapo wa makipa bora kabisa katika historia ya soka."

Manuel Neuer anatarajiwa kurejea dimbani kesho katika mchezodhidi ya Darstadt
Manuel Neuer anatarajiwa kurejea dimbani kesho katika mchezodhidi ya DarstadtPicha: Laci Perenyi/IMAGO

Nafasi ya unahodha ya Neuer ambaye ameichezea Bayern mechi  500 tangu asajiliwe kutoka Schalke 04 mwaka 2011, kwenye timu ya taifa ya Ujerumani  imechukuliwa kiungo wa Barcelona, ​​Ilkay Gundogan.

Soma zaidi:Guirassy avunja rekodi za Bundesliga

 Hata hivyo, nyota huyo ameonesha nia yake ya kurejea katika kikosi cha timu ya taifa na lengo lake kuu ni kusimama kati lango wakati wa mashindano ya  Euro 2024, mashindano ambayo Ujerumani itakuwa mwenyeji.

Bayern wanaingia wikendi hii wakiwa safi baada kutoka kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Galatasaray mjini Istanbul katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa lakini wako katika nafasi ya tatu kwenye Bundesliga baada ya mechi nane, pointi mbili nyuma ya vinara Bayer Leverkusen.

Darmstadt iliyopanda daraja msimu huu ilikuwa imepata ushindin katika mechi tatu mfululizo kabla ya kucharazwa 3-1 nyumbani na RB Leipzig katika mechi yao ya mwisho.